Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran: Shahidi Nasrallah aligeuza Hizbullah kuwa ngome imara

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran amesema Shahidi Sayyid Hassan Nasrallah alikuwa kiongozi wa muqawama (mapambano ya Kiislamu), mwanazuoni wa mujahidina na kamanda shupavu, shujaa na mbunifu ambaye aliigeuza harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon kuwa ngome imara.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Iran Press, Hujjatul Islam Mohammad Hassan Abu Tarabi Fard amesema katika khutba ya Swala ya Ijumaa mjini Tehran kwamba: Natoa salamu za rambirambi kwa kuwasili siku ya 40 ya Sayyid Hassan Nasrallah.

Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran ameongeza kuwa: Shahidi Nasrallah alikuwa ni mtu aliyegeuza mhimili wa muqawama kuwa nembo ya nguvu na kusimama kidete umma wa Kiislamu na umma Kiarabu dhidi ya utawala wa Kizayuni, uistikbari wa kimataifa na Marekani na akiwa muungaji mkono mwenye nguvu wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiisalmu aliweza kubadilisha milinganyo ya kisiasa katika eneo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Hujjatul Islam Abu Tarabi Fard ameashiria kumbukumbu ya mhandisi mahiri na mujahid asiyechoka ambaye ni baba wa tasnia ya makombora nchini Iran, shahidi Jenerali Brigedia Jenerali Tehrani Moghadam. Amesema matokeo ya juhudi za miaka mingi za msomi huyo na washirika wake ni uwezo wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambao ulidhihirika katika miezi ya hivi karibuni katika operesheni mbili za kijeshi za Ahadi ya Kweli dhidi ya utawala wa Kizayuni.