Kamal Kharrazi, Mkuu wa Baraza la Kistratejia la Mahusiano ya Nje la Iran amesema, kuna muelekeo wa Jamhuri ya Kiislamu kuongeza umbali wa masafa yatakakofika makombora yake, akionya kuwa Tehran inaweza kubadilisha mwongozo wake wa kijeshi iwapo itakabiliwa na kitisho cha kuhatarisha uwepo wake.
Dakta Kharrazi ameyasema hayo katika mahojiano na televisheni ya al-Mayadeen ya Lebanon na akatamka bayana: “iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakabiliwa na kitisho cha kuhatarisha uwepo wake, bila shaka tutabadilisha sera ya mwongozo wetu wa kijeshi” .
Amesisitiza kuwa Iran inao uwezo wa kuunda silaha za nyuklia, lakini kinachoizuia ni fatwa (amri ya kidini) iliyotolewa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei inayokataza utengenezaji wa silaha za maangamizi ya halaiki.
“Sasa hivi tunao uwezo unaohitajika wa kutengeneza silaha [za nyuklia], na kizuizi pekee kilichopo ni fatwa ya Kiongozi ambayo inakataza utengenezaji wa silaha za nyuklia.”

Kuhusu umbali wa masafa yanakofika makombora ya Iran, Mkuu wa Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Nje la Iran amesema: “hadi sasa tumezingatia wasiwasi wa Wamagharibi, hasa wa Ulaya. Lakini kama na wao hawatozingatia wasiwasi wetu, hususan kuhusu suala la umoja wa ardhi yote ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hakuna sababu ya sisi kuendelea kuzingatia wasiwasi wao. Kwa hiyo, upo uwezekano wa kuongezeka masafa yatakakofika makombora ya Iran.”
Akizungumzia mashambulizi mabaya yaliyofanywa hivi karibuni na utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye maeneo ya kijeshi nchini Iran, Kharrazi amesema, hakuna shaka yoyote Jamhuri ya Kiislamu itajibu uchokozi huo katika wakati sahihi na kwa njia sahihi.
Aidha, amebainisha kuwa Iran haipendelei kupanuliwa vita katika eneo zima, lakini akasisitiza kwa kusema, “tuko tayari kwa vita kamili”…/