Khaligraph Jones kivutio katika Bongofleva

Dar es Salaam, Hakuna ubishi kuwa Msanii wa Hip Hop kutoka nchini Kenya, Khaligraph Jones amekuwa kivutio kikubwa kwa wasanii wa Bongofleva kwa miaka ya hivi karibuni jambo linalofanya kila msanii kutaka kufanya naye wimbo.

Khaligraph ambaye mwaka 2018 alishinda tuzo ya African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kama Msanii Bora wa Hip Hop Afrika, hadi sasa ameshirikishwa kwenye nyimbo na wasanii zaidi ya 15 kutoka Tanzania. Hawa ni baadhi yao; 

1. Rosa Ree ft. Khaligraph Jones –  Up In The Air Remix

Kipindi Rosa Ree yupo chini ya usimamizi wa lebo ya The Industry yao Navy Kenzo, ndipo kolabo hii ilifanyika, pia ukaribu wao ililetwa zaidi walipokuwa mabalozi wa kinywaji cha Belaire.
Wimbo huo ambao ulitoka Juni 2016 ndio ilikuwa wa kwanza kwa Rosa Ree kumshirikisha msanii mwingine tangu kuanza muziki, ndipo wakafuata wengine kama Billnass na Rapa Emtee wa Afrika Kusini.

2. Young Killer ft. Khaligraph Jones – Shots

Mara baada ya Young Killer kusaini kuwa chini ya Wanene Entertainment ndipo lebo hiyo ilimleta Khaligraph Jones nchini na kufanya video ya wimbo ‘Shots’ ambao tayari walikuwa wameurekodi kitambo.

Hii ilikuwa ni kolabo ya kwanza ya kimataifa kwa Young Killer, baadaye alimshirikisha msanii mwingine wa Kenya, Dela katika wimbo wake uitwao Wakipekee. 

3. Nikki Mbishi ft. Khaligraph Jones –  Baba Yao

Nikki Mbishi anatambulika kama msanii wa kwanza Bongo kufanya kolabo na Khaligraph Jones, ni mwaka 2014 walipoachia wimbo uitwao Baba Yao. 

Baadaye Nikki alikuja kumshirikisha Rapa mwingine wa Kenya, Collo katika wimbo wake ‘Toast To Life’ ambao Vanessa Mdee kasikika pia. Hata hivyo nyimbo zote hizi mbili hazikufanyiwa video hadi sasa. 

4. Christian Bella ft. Khaligraph Jones – Ollah 

Mara baada ya Bella kusikika kwenye ngoma za wakali wa Hip Hop Bongo za Fid Q (Roho) na Weusi (Nijue), aliona michano inafaa katika muziki wake ndipo akamtafuta Khaligraph na kutoa wimbo huo, Ollah (2017). 

Huyu alikuwa msanii wa pili Bongo anayeimba kufanya kolabo na Khaligraph baada ya Rayvanny, pia katika kolabo yao kuna sauti (back vocal) za Ruby na Nandy walizoingiza kwa nyakati tofauti.

5. Chin Bees ft. Khaligraph Jones – Kababaye Remix 

Naye Chin Bees akiwa chini ya Wanene Entertainment aliamua kufanya remix ya nyimbo zake mbili zilizokwisha kufanya vizuri kwa kuwashirikisha wasanii wakubwa Afrika Mashariki.

Ndipo Khaligraph Jones akasikika kwenye ngoma ‘Kababaye Remix’, huku wakali wengine toka Kenya, Wyre na Nazizi wakisikika kwenye wimbo wake mwingine uitwao Nyonga Nyonga Remix.

6.  Stereo ft. Khaligraph Jones – Mpe Habari Remix

Wakati Rich Mavoko yupo chini ya WCB Wasafi aliandaliwa mpango wa kufanya kazi na wasanii wa Hip Hop Bongo, ndipo akashirikishwa na Stereo kwenye wimbo ‘Mpe Habari’ ambao ulifanya vizuri.

Kufanya vizuri kwa wimbo huo waliamua kutoa na remix yake ndipo Khaligraph Jones akachukua nafasi, huko wasanii wa Bongo waliosikika wakiwa ni Billnass, Stamina na Jay Moe. 

7. Rostam ft. Khaligraph Jones – Now You Know

Kundi hili la Hip Hop Bongo linaloundwa na Roma na Stamina, lilisafiri hadi Kenya kwenda kurekodi wimbo ‘Now You Know’ wakimshirikisha Khaligraph Jones, pia video ya ngoma hiyo ilifanyika nchini humo.

Rostam ambao mwaka 2020 walichaguliwa kuwania tuzo ya MTV Africa Music Awards (MAMAs) katika kipengele cha Kundi Bora la Muziki, hadi sasa hawajamshirikisha msanii mwingine yeyote kutoka nje ya Tanzania. 

8. Ommy Dimpoz ft. Khaligraph Jones – Kata Remix

Ngoma hii iliyotoka Januari 2020 ndio kolabo ya mwisho kwa Ommy Dimpoz na msanii kutoka Kenya baada ya Khaligraph, katika wimbo wenyewe (original version) Ommy Dimpoz alimshirikisha Nandy pekee na kufanya vizuri.

Lilipokuja suala la remix ndipo Khaligraph Jones akachukua namba pamoja na msanii mwingine wa Kenya, Redsan, pia Nandy aliendelea kuwepo. Tofauti na ilivyokuwa kwa Chin Bees na Stereo, Ommy Dimpoz aliamua kutoa video ya wimbo huo kama alivyofanya Rosa Ree kwenye Up In The Air Remix. 

9. Harmonize ft. Khaligraph Jones & DJ Seven – Die 

Katika albamu yake ya kwanza iliyotoka Machi 14, 2020 ikiwa na ngoma 18, Harmonize amemshirikisha Khaligraph Jones katika wimbo, Die akiwepo na DJ Seven pia.

Huyu anakuwa msanii wa pili Bongo aliyetolewa na WCB Wasafi kimuziki kufanya kazi na Khaligraph Jones baada ya Rayvanny aliyeshirikiana na Rapa huyo katika ngoma, Chalii ya Ghetto

10. Alikiba ft. Khaligraph Jones – Habibty

Oktoba 4, 2021 Alikiba aliachia albamu yake ya tatu, ‘Only One King’ yenye nyimbo 16, ikiwa ni miaka 11 tangu alipoachia albamu yake ya kwanza, Cinderella iliyotoka mwaka 2007.

Katika albamu hiyo wimbo namba 10 uitwao Habibty amemshirikisha Khaligraph Jones, pia wasanii wengine wa Kenya kama Nyashinski  na kundi la Sauti Sol ameshirikishwa. 
Wasanii wengine wa Bongofleva waliofanya kazi na Khaligraph