
MZUNGUKO wa mwisho wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu wa 2024-2025 unahitimishwa leo Mei 20, 2025 kwa mechi tano kuchezwa huku Mlandizi Queens na Gets Program zikiwa tayari zimeshuka daraja.
Katika kuhitimisha msimu, michezo miwili ambayo Gets Program dhidi JKT Queens na Alliance Girls dhidi Simba Queens, itaenda kuamua bingwa wa ligi hiyo kutokana na msimamo ulivyo.
JKT Queens na Simba Queens zimelingana pointi kwenye msimamo zote zikiwa na 44 baada ya kucheza mechi 17 zikitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
Ili Simba Queens itetee ubingwa wa ligi hiyo, inatakiwa kushinda dhidi ya Alliance Girls huku ikiombea JKT Queens ipoteze au kutoka sare dhidi ya Gets Program.
JKT Queens inausaka ubingwa wa ligi hiyo ilioupoteza msimu uliopita huku ikifukuzia rekodi ya Simba Queens inayoongoza kubeba mara nne. Kwa sasa JKT Queens imeshinda ubingwa huo mara tatu.
Rekodi za mabingwa wa Ligi Kuu Wanawake zinaonyesha hivi; Mlandizi Queens (2017), JKT Queens (2017/2018), JKT Queens (2018/2019), Simba Queens (2019/2020), Simba Queens (2020/2021), Simba Queens (2021/2022), JKT Queens (2022/2023) na Simba Queens (2023/2024).
MECHI ZA MWISHO WPL
Alliance Girls 🆚 Simba Queens
🕓 Saa 10 Jioni
🏟️ TFF Center Kigamboni
Gets Program 🆚 JKT Queens
🕓 Saa 10 Jioni
🏟️ Jamhuri Stadium Dodoma
Yanga Princess 🆚 Ceasiaa Queens
🕓 Saa 10 Jioni
🏟️ KMC Complex
Mashujaa Queens 🆚 Bunda Queens
🕓 Saa 10 Jioni
🏟️ TRA Mivinjeni Dar
Fountain Princess 🆚 Mlandizi Queens
🕓 Saa 10 Jioni
🏟️ Tanzanite Kwaraa