
UNAIKUMBUKA lile jambo la tuhuma ya beki wa zamani wa Simba na Yanga, Hassan Kessy hadi ikazaliwa ‘kampa kampa’ Ngoma na mashabiki wa Jangwani wakachapisha jezi zenye maneno hayo, ilikuwa ni dabi ya msimu wa 2015/16.
Mwanaspoti limekwenda kuchimba undani wa ishu hiyo kwa kumtafuta mhusika ili kufafanua ilikuaje hadi akawa anatuhumiwa alichukua rushwa ili Simba ifungwe mechi hiyo ambayo Msimbazi walishinda mabao 2-0 na wakawa na mwendelezo wa kuchukua mataji misimu mitatu mfululizo.
Kessy amefafanua kwa nini alirudisha mpira kwa kipa Vincent Angban, alisema yalikuwa makubaliano baada ya mambo kwenda ndivyo sivyo akageuziwa kibao.
“Kwanza tuanze na hiyo ya uwanjani ambayo ilizaa kampa kampa tena. Kipa aliniambia nimrudishie mpira alishindwa kuuwahi ndipo Donald Ngoma akafunga. Baada ya kufungwa nikaonekana nina makosa kwa nini nirudishe mpira nyuma badala ya kupiga mbele, nikawajibu viongozi kipa alisema nimrudishie, kipa alipoulizwa akaniruka,” amesema Kessy na kuongeza:
“Kabla ya mchezo nilianza kuambiwa mambo mengi ya kunitoa mchezoni. Kuna kiongozi aliniambia pesa ulizochukua Yanga zitakutokea puani nilikuwa sielewi ilikuaje, ila ajabu kuna kiongozi akawa anawashawishi baadhi ya wachezaji wachukue pesa nikiwemo mimi mwenyewe, na alisema kabisa tutafungwa mabao mawili, beki mmoja wa kati atapewa kadi nyekundu na mwamuzi atakuwa nani.
“Yalikuwepo mambo mengi pia nikawa nalazimishwa kusaini mkataba ulikuwa unaelekea mwishoni, nikawa nawaambia siwezi kufanya hivyo wakati hayupo meneja wangu alikuwa ni Tipo. Hilo likawa linazidi kunifanya nionekane nipo upande wa Yanga lakini ukweli haikuwa hivyo.”
Amesema, “sitaki kuweka wazi ni kiongozi gani, ila nakumbuka kipindi hicho ndio alikuwa anapanga waamuzi, aliwaita mabeki wawili na kuwaambia ni mwamuzi gani atachezesha mchezo wao wa dabi na watapoteza kwa mabao mawili na mmojawapo kati ya hao atapata kadi nyengundu. Baada ya dakika 90 ndicho kilichotokea, hivyo mengi yanazungumzwa ila ukweli ni kwamba ule mchezo na tukio lililotokea haikuwa mipango ni sehemu ya mchezo.”
DABI JUMAMOSI
Akizungumzia mchezo wa Jumamosi, Kessy amesema asilimia 60 anaipa Yanga ushindi huku akiweka wazi sababu kuwa timu hiyo ni bora kila eneo, lakini wapinzani wao Simba wana ubora kuanzia kiungo na ushambuliaji wakiwa na mpira.
“Yanga imekamilika kila idara tofauti na Simba wao kuanzia eneo la kiungo ni wazuri, hasa wakiwa na mpira. Lakini wakipoteza huoni wakicheza vizuri kama mabingwa watetezi watakosa matokeo basi mpira utaisha kwa sare,” amesema.
“Mchezo huo unaamua ubingwa kama Yanga atapata matokeo atajihakikishia nafasi ya kutetea taji, hivyo watacheza kama wanalisaka. Wakati huohuo Simba ikiibuka na ushindi itakuwa inasikilizia matokeo ya kiporo chake na Dodoma Jiji kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kutwaa taji baada ya kukosa misimu mitatu mfulululizo.”