
Dar es Salaam. Kesi mbili ikiwemo ya kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni zinazomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, leo Jumatatu, Mei 19, 2025 zitaunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo, kesi nyingine inayomkabili kiongozi huyo ni kesi ya uhaini.
Hata hivyo, leo Jumatatu Mei 19, 2025, kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa YouTube, imeitwa kwa ajili ya Serikali kumsomewa hoja za awali (PH) ili kesi hiyo iweze kuendelea na usikilizwaji wa mashahidi.
Kusomewa kwa hoja za awali kwa mshtakiwa huyo kunatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.
Wakati hayo yakitarajiwa kufanyika, tayari Mahakama hiyo katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo imetoa hati ya kumuita mshtakiwa kutoka gerezani kuletwa mahakamani hapo ili aje asikilize kesi yake ili kuruhusu ndugu, jamaa, marafiki na wanachama wa chama chake waweze kuhudhuria.
Uamuzi huo ulitolewa Mei 6, 2025 na Hakimu Mkazi Mwandamiizi, Geofrey Mhini, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa uamuzi iwapo mwenendo wa kesi hiyo usikilizwe kwa njia ya mtandao au mshtakiwa apelekwe mahakamani.
Katika uamuzi wake, alitoa maelezo matano, ikiwemo Mahakama hiyo kuridhia, mshtakiwa huyo kupelekwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusikiliza kesi yake ya kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa YouTube.
Pia, kesi hiyo isikilizwe Mahakama ya wazi ili kila mmoja aweze kuhudhuria.
Vilevile, mshtakiwa huyo apelekwe mahakamani hapo siku hiyo kwa ajili ya kwenda kusomewa hoja za awali (PH) ambazo zitasomwa na upande wa mashitaka.
Maelekezo mengine yalikuwa ni watu na wafuasi wa chama hicho wanaokwenda kusikiliza kesi hiyo wasikilize kwa utulivu na watunze amani ndani na nje ya Mahakama.
Mashitaka yake ya kuchapisha taarifa za uongo
Lissu ambaye yupo rumande Gereza la Ukonga, anakabiliwa mashitaka matatu ya kutoa taarifa za uongo, kinyume cha sheria
Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka hayo ya kutoa taarifa za uongo mitandaoni, kinyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015, kifungu cha 16.
Mashitaka hayo yote matatu ni ya kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa Youtube, akidaiwa kutenda makosa hayo Aprili 3, 2025 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kulaghai umma.
Katika shitaka la kwanza, Lissu anadaiwa kuchapisha maneno ambayo yanasomeka…
“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 wagombea wa Chadema walienguliwa’ kwa maelekezo ya Raisi”, wakati akijua maneno hayo ni ya uongo na ya apotosha umma.
Shitaka la pili anadaiwa siku hiyo alichapisha taarifa za uongo na za kupotosha umma kuwa:
“Mapolisi wanatumika kuiba kura wakiwa na vibegi.”
Katika shitaka la tatu anadaiwa siku hiyohiyo alichapisha taarifa kuwa:
“Majaji ni Ma-CCM, hawawezi kutenda haki, wanapenda wapate teuzi na kuchaguliwa kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa.
Wakati huohuo kesi ya uhaini inayomkabili mshtakiwa huyo nayo itatajwa mahakamani hapo
Lissu ambaye alishawahi kuwa rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), anakabiliwa na shitaka hilo, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.
Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Franco Kiswaga na ilipangwa kutajwa leo ili kuangalia iwapo upelelezi wa shauri hilo umekamilika au laa, kutokana na Hakimu huyo kuelekeza upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi kwa wakati.
Hata hivyo, kesi hiyo ya uhaini mara zote imekuwa ikisikilizwa kwa njia ya mtandao lakini kutokana na mshtakiwa huyo kupelekwa mahakamani siku hiyo kusikiliza kesi ya kuchapisha taarifa za uongo, hiyo pia itasikizwa mahakama ya wazi.
Shitaka la uhaini
Katika kesi ya msingi, Lissu anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 3, 2025 ndani ya jiji la Dar es Salaam, ambapo kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuandika maeneo yafuatayo:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kikinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kwa mara ya kwanza, Lissu alifikishwa mahakamani hapo Aprili 10, 2025 na kusomewa kesi mbili ikiwemo ya uhaini.