
Kigoma. Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imepokea fomu ya matokeo ya uchahuzi wa mwenyekiti wa Mtaa wa Livingstone, Kata ya Kasingirima, Manispaa ya Kigoma Ujiji, kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mwombaji (mlalamikaji) katika shauri la kupinga uchaguzi huo.
Mahakama hiyo imeipokea fomu hiyo inayoonesha taarifa muhimu baada ya kutupilia mbali pingamizi la Serikali iliyopinga fomu hiyo isipokewe kuwa kielelezo cha ushahidi wa mwombaji katika shauri hilo kwa madai kuwa imekiuka matakwa ya kisheria.
Hata hivyo, Hakimu Aristida Tarimo anayesikiliza shauri hilo katika uamuzi wake baada ya kusikiliza hoja za pande zote amekubaliana na hoja za mawakili wa utetezi na akazikataa hoja za upande wa wajibu maombi (walalamikiwa)
Shauri hilo limefunguliwa na aliyekuwa mgombea wa nafasi ya mwenyekiti wa mtaa huo wa Livingstone, Kata ya Kasingirima katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji, vijiji mwaka 2024 kupitia Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Luma Akilimali.
Wajibu maombi (walalamikiwa shauri hilo) linalosikilizwa na Hakimu A. V Tarimo ni aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo, Mawazo Kiembe, msimamizi msaidizi wa uchaguzi Mtaa Livingstone pamoja na msimamizi wa uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa).
Akilimali anadai mchakato wa uchaguzi huo wenyewe haukuwa huru na wa haki kakiuka kanuni zilizowekwa na hivyo kuifanya kuwa batili, kutokana na kasoro zilizojitokeza.
Amebainisha kasoro hizo ni pamoja na mchakato wa uandikishaji wapiga kura kutokufanyika kwa mujibu wa kanuni, ongezeko la wapigakura, mtendaji wa kata kuharibu uchaguzi kwa kuingia kituoni na kura alizozichangaya kwenye kura zilizokuwa zinahesabiwa.
Nyingine ni baadhi ya watu kupiga kura zaidi ya moja huku wakisadiwa na msimamizi msimaidizi, sanduku la kura za mwenyekiti kuwekwa mafichoni ambako mawakala hawakuwa wanaona waliokuwa wanatumbukiza kura, watu wasiokuwa wakazi kupiga kura na kuingizwa kura bandia.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, imuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku 14 na ndani ya siku 60 uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo ufanyike.
Pingamizi na mawakili walivyochuana kwa hoja
Wakati akitoa ushahidi wake, akiongozwa na Wakili wake Eliutha Kivyiro ameiomba mahakama hiyo ipokee fomu hiyo namba 8A ya matokeo ya mwenyekiti wa mtaa, iwe kielelezo cha ushahidi wa madai yake, ndipo mawakili wa utetezi wakaipinga.
Wakili wa Serikali, Mathew Fuko amedai fomu hiyo ni nakala kivuli (photocopy) na upande wa mwombaji hawakutoa taarifa ya kusudio la kutumia nyaraka kuwasilisha nyaraka ya aina hiyo kama Sheria ya Ushahidi inavyoelekeza kuhusu uwasilishaji wa nyaraka vivuli mahakamani.
Sababu ya pili ambayo amesema ni mbadala wa sababu ya kwanza (kama Mahakama itaona kuwa fomu hiyo ni halisi (siyo nakala kivuli), amedai kuwa uwasilishaji wake haujazingatia matakwa ya sheria hiyo.
Amefafanua hiyo ni nyaraka ya umma ambayo ili iweze kutumika ilipaswa iwe imethibitishwa na mamlaka husika kuwa ni halisi na sahihi, kwa mujibu wa kifungu cha 85 cha Sheria ya Ushahidi, na kwamba kwa nyaraka hiyo mamlaka husika ni mamlaka ya uchaguzi huo.
Akijibu hoja hizo wakili Kivyiro amepinga pingamizi na hoja hoja za pingamizi hilo zilizotolewa na Wakili Fuko, kwanza akidai kuwa fomu hiyo si nakala kivuli bali ni nakala halisi.
“Mawakili wa Serikali hawajasema ni kipi kimewafanya waseme hii ni kivuli bali wameiangalia tu. Mheshimiwa Hakimu na sisi kwa kuangalia tu hiyo ni nakala halisi. Hata wewe Mheshimiwa ukiiangalia tu hii ni nakala halisi,” amesema Wakili Kivyiro.
Kuhusu hoja ya kuwa kwa kuwa ni nyaraka ya umma ilipaswa kuthibitishwa, amedai kuwa Wakili Fuko hajasema ni kifungu gani cha sheria ambacho kinaizuia nyaraka ya umma halisi kuwa katika mikono ya raia wala sheria gani inayoelekeza kuwa raia anapaswa kupewa nakala kivuli tu.
Hivyo amesema kuwa takwa la kifungu cha 85 cha Sheria ya Ushahidi, kuthibitisha nyaraka vivuli haliwezi kutumika katika mazingira ya kesi hiyo alisisitiza kuwa kwa kuwa nyaraka hiyo ni hali nasi haipaswi kuthibitishwa.
Hakimu Tarimo katika uamuzi wake kwanza amekubaliana na hoja za wakili Kivyiro kuwa fomu hiyo ni nakala halisi na si kivuli.
Amesema baada ya kurejea na kuzingatia hoja za pande zote, kesi rejea zilizorejewa na mawakili na kifungu cha 85 cha Sheria ya Ushahidi Mahakama inaamua kuwa katika kifungu hicho hakuna mahali ambapo imekataa nakala halisi isipokewe.
“Kwa kuzingatia hoja za Kivyiro kuwa hiyo ni nakala halisi sioni kama mahakama hii inakatazwa kupokea nakala hii halisi,” amesema Hakimu Tarimo na kuhitimisha:
“Kwa kusema hivyo natupilia mbali pingamizi hili na nakubali kielelezo hiki kama kielelezo cha kwanza cha upande wa mwombaji.”
Baada ya uamuzi huo shahidi huyo ameendelea na ushahidi wake.