Kesi ya rasilimali Chadema ni pingamizi juu ya pingamizi

Dar es Salaam. Kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali inayokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imegubikwa na pingamizi, kila upande ukiuwekea mwingine.

Kesi hiyo, inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imetajwa mara ya pili leo Jumatatu, Mei 12, 2025.

Jopo la mawakili wa Chadema linaloongozwa na Dk Rugemeleza Nshala limeieleza Mahakama kuwa limeshawasilisha majibu ya utetezi na limeweka pingamizi lenye hoja tisa dhidi ya kesi hiyo.

Mahakama imeelekeza kusikilizwa kwanza pingamizi kabla ya kesi ya msingi. Pingamizi zitasikilizwa kwa njia ya maandishi.

Mahakama imeelekeza Chadema kuwasilisha hoja za maandishi kuhusu pingamizi Mei 23, na wadai watajibu hoja hizo Mei 30. Iwapo kutakuwa na majibu ya nyongeza, Chadema imetakiwa kuyawasilisha Juni 6, 2025.

Mahakama imepanga kutoa uamuzi wa pingamizi za Chadema Juni 10, 2025.

Licha ya kesi ya msingi, wadai wamefungua maombi madogo ya zuio wakiomba Mahakama itoe amri dhidi ya Chadema kutofanya shughuli za siasa na kutokutumia mali za chama hicho hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa.

Chadema imeweka pingamizi dhidi ya maombi hayo, huku wadai nao wakiweka pingamizi dhidi ya kiapo kinzani cha Chadema.

Jopo la mawakili wa wadai linaoongozwa na Mulamuzi Byabusha, limeieleza Mahakama limeibua hoja tano za pingamizi dhidi ya kiapo kinzani cha wadaiwa.

Jaji Mwanga ameelekeza pingamizi dhidi ya maombi hayo ya zuio na shauri la maombi ya zuio yasikilizwe Juni 10, 2025 kwa mdomo.

Kesi hiyo imefunguliwa na Said Issa Mohamed, aliyejitambulisha kuwa mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis, na Maulida Anna Komu, ambao wamejitambulisha kuwa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.

Wadaiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Mwanga, Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema, ikiwa mdaiwa wa kwanza, na Katibu Mkuu wa Chadema, akiwa mdaiwa wa pili.

Katika kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025, wadai wanaiomba Mahakama itamke na kutoa amri kumuamuru kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na katiba ya chama hicho.

Wamechukua hatua hiyo wakidai kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Pia wanadai kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia, pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga Muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *