
Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili msanii wa uigizaji Joyce Mbaga (32), maarufu Nicole Berry na mwenzake Rehema Mahanyu (31), itatajwa leo Jumatatu Machi 24, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni inayoketi Kinondoni.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Machi 10, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu.
Siku hiyo, Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu aliwasomea mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhani Rugemalira.
Katika mashitaka yao, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai 2024 na Machi 2025 ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashitaka matatu la kwanza la kuongoza genge la uhalifu, kwa lengo la kujipatia fedha.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia faida kwa kupokea amana au miamala kutoka kwa jamii bila kupata leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika shitaka la pili washtakiwa wote wanadaiwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025 wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walipokea amana ya Sh185.51 milioni kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni.
Shitaka la tatu wanadaiwa kuendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.
Hata hivyo, washtakiwa hao wapo nje kwa dhamana baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.
Miongoni mwa masharti hayo ni kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani sawa na nusu ya kiasi cha fedha wanazodaiwa kukusanya kutoka kwa umma.
Hakimu Rugemalira alifafanua nusu ya fedha hiyo ni Sh92. 75 milioni hivyo kila mmoja wao atatakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh46.37 milioni.
Pia, Hakimu Rugemalira aliwataka washtakiwa hao kuwa na wadhamini kila mmoja, wenye barua za utambulisho kutoka serikali za mitaa na kama ni mwajiriwa awasilishe barua ya ofisi yake.