KESI YA MAUAJI YA KIFAMILIA: Shahidi aeleza watuhumiwa, mama, mwanaye walivyotiwa mbaroni

KESI YA MAUAJI YA KIFAMILIA: Shahidi aeleza watuhumiwa, mama, mwanaye walivyotiwa mbaroni

Dar es Salaam. Naibu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Iringa, Mrakibu wa Polisi, Michael Sabhai ameeleza namna washtakiwa katika kesi ya mauaji ya kifamilia walivyokamatwa kwa tuhuma za mauaji hayo.

Sabhai amebainisha hayo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, na Hakimu Mkazi mwenye mamlaka ya ziada Mary Mrio.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Sophia Mwenda na mtoto wake wa kiume, Alphonce Magombola. Wote wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya mwanafamilia, Beatrice Magombola, Desemba Mosi, 2020, nyumbani kwa marehemu Beatrice, eneo la Kijichi, wilayani Temeke, Dar es Salaam.

Wanadaiwa kuwa siku ya tukio, Alphonce alikuwa amemshikilia mikono dada yake Beatrice kisha mama yake, Sophia akamchoma kwa kisu chini ya titi la kushoto

Wanadaiwa kuwa baada ya kutekeleza mauaji hayo walikwenda kuutupa mwili eneo la Zinga, wilayani Bagamoyo, kichakani.

Washtakiwa hao wanadaiwa kuwa waliamua kutekeleza mauaji hayo  katika jitihada za kutaka kumzuia  mwanafamilia huyo kwenda kutoa ushahidi kwenye kesi ya nyumba ya familia iliyouzwa na washtakiwa hao huko jijini Mbeya. 

Katika ushahidi wake,  jana, Mei 20, 2025, Sabhai  ambaye ni shahidi wa tisa wa upande wa mashitaka ameieleza Mahakama hiyo kuwa washtakiwa hao walikamatwa kutokana na taarifa kutoka kwa msiri kuhusu kupotea kwa Beatrice, mwaka mmoja na miezi mitatu  baadaye.

Kwa mujibu wa ushahidi wake alioutoa akiongozwa na Wakili wa Serikali, Daisy Makakala wakati wa washtakiwa hao walipokamatwa alikuwa DRCO Mkoa wa Kipolisi Kinondoni Kanda Maalumu Dar e s Salaam.

Machi 16, 2022 saa 2 usiku akiwa ofisini kwake Oysterbay Polisi alielekezwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Ramadhani Kingai ( kwa Sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai – DCI) kufungua jalada la uchunguzi wa kupotea kwa mtu aitwaye Beatrice Douglas Magombola.

Kingai alimweleza Sabhai kuwa amepokea  taarifa kutoka kwa msiri kuwa kuna mtu huyo, Beatrice  amepotea kwa zaidi ya mwaka.

Kingai, alimweleza Sabhai kuwa msiri huyo amemwambia  mama yake Beatrice aitwaye  Sophia Alphonce  Mwenda (mshtakiwa wa kwanza) na mdogo wake Beatrice, Alphonce Douglas Magombola (mshtakiwa wa pili) wamekuwa wakitoa taarifa tata kwamba mara yuko Canada mara Afrika Kusini kwenye matibabu.

Sabhai baada ya kufungua jalada hilo aliwasiliana na msiri huyo ili kuwapata ndugu wa Beatrice kwa mahojiano akitaka kusikia wao wanajua nini kuhusu kupotea kwa Beatrice.

Hivyo aliunda timu iliyoongozwa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi,  Tura  ambaye  alimpatia mawasiliano ya msiri kwa ajili ya kuwakamata Alphonce na mama yake, Sophia.

Kesho yake Machi 17,  saa 10:45 asubuhi Tura alimpigia simu Sabhai na kumjulisha kuwa walikuwa  wamefanikiwa kumkamata Alphonce huko Bunju.

Alphonce alipofikishwa  kituoni Sabhai  alimuelekeza Ditektivu Deusdedith amuhoji kuhusiana na mahali aliko Beatrice.

Muda wa saa 3 Deusdedith  alimpigia simu Sabhai akamueleza kuwa Alphonce amesema kuwa mtu huyo, Beatrice  walikuwa wamekwishamuua, yeye Alphonce  na mama yake.

SP Sabhai alielekeza mtuhumiwa huyo awekwe mahabusu kisha lifunguliwe jalada la mauaji na yeye Sabhai alimjulisha RPC Kingai kuhusu taarifa hizo.

Kesho yake, Machi 18, 2022, Sabhai  alimwandaa askari kwa ajili ya kwenda kumkamata mtuhumiwa Sophia ambaye alipata taarifa kuwa alikuwa anaishi Mbagala, na saa 11 jioni, askari huyo  alimjulisha kuwa wameshamkamata na wamemkamatia Sinza.

Sophia baada ya kufikishwa kituoni Oysterbay,  Sabhai  alimwelekeza Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Nicolaus amuhoji mtuhumiwa  kuhusiana na mauaji ya Beatrice.

Kutokana na maelezo ya watuhumiwa hao kukiri kumuua Beatrice ni kwamba walikwenda kumtupa Bagamoyo, Machi 19, 2022, Sabhai  alimpa maelekezo Inspekta James kuambatana na wapelelezi wa jalada hilo Deusdedith kwa ajili ya kufanya uchunguzi  zaidi.

Machi 25, 2022 mshtakiwa wa pili, Alphonce alikwenda kuwaonyesha mahali walikotupa mwili wa Beatrice.

Kutokana na uchunguzi walipata taarifa kuwa mwili ulikuwa umezikwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo.

Hivyo walifanya  taratibu za kupata kibali cha kwenda kufukua mwili ule wa ajili ya vipimo ukiwemo uchunguzi wa  vinasaba (DNA).

Licha kukamatwa Machi, 2022, washtakiwa walifikishwa mahakamani na kusomewa shitaka hilo, Julai 15, 2022, miezi minne baadaye.

Sabhai ameieleza Mahakama kuwa hali hiyo ilitokana na kuchelewa kukamilika kwa uchunguzi kwa kuwa ulihusisha na taasisi nyingine.

Akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa utetezi, Hilda Mushi shahidi huyo amesema kuwa hajatoa nyaraka mahakamani kuthibitisha nani aliwapa mamlaka Kinondoni kufanya uchunguzi wa tukio ambalo halikufanyika mkoani  kwake.

Kesi hiyo inaendelea leo Mei 21, 2025 kwa upande wa Jamhuri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *