KESI YA FATMA KARUME: Mwanasheria Mkuu, Kamati ya mawakili wapewa siku 60

Arusha. Mahakama ya Rufani imekubali maombi ya Serikali ya ruhusa ya kukata rufaa kupinga wakili wa kujitegemea, Fatma Karume kurejeshwa kufanya shughuli zake za uwakili Tanzania Bara.

Mahakama hiyo imetoa muda wa siku 60 kuanzia jana Aprili 15,2025 kwa ajili ya kukata rufaa hiyo.

Mahakama hiyo ilikubali shauri la maombi hayo ikiomba ruhusa kukata rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomrejeshea uwakili Karume, aliofutiwa na kamati ya mawakili iliyomtia hatiani kwa kosa la ukiukwaji wa maadili ya kitaaluma.

Awali, Serikali ilifungua maombi hayo Mahakama Kuu ikiomba ruhusa ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomrejeshea Karume uwakili, lakini Mahakama Kuu iliikataa, ndipo Serikali ikaenda kuomba ruhusa Mahakama hiyo ya Rufani.

Waombaji katika maombi hayo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Kamati ya Mawakili, ambapo Jaji Lilian Mashaka wa Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, ametoa uamuzi huo jana Aprili 15,2025.

Maombi hayo ya kuongezewa muda yaliyotolewa chini ya kanuni za 10, 4 (2) (b) na (c) na 48 (1) za Kanuni za Mahakama ya Rufani ya Tanzania za mwaka 2019.

Jaji Mashaka amesema akirejea kifungu cha 19 cha hati ya kiapo, Wakili Rumisha alieleza kuwa, waombaji hawakuweza kuwasilisha rekodi ya rufaa kwa sababu haki ya kukata rufaa ilikuwa chini ya kuomba na kupata kibali cha kukata rufaa, ambacho ingawa kiliombwa lakini kilipitwa na mabadiliko ya sheria yaliyotupilia mbali matakwa hayo.

Amesema sababu nyingine inayoombwa kwa ajili ya kuongezwa ni kwamba, uamuzi wa Mahakama ya juu una dosari na uvunjaji wa sheria kuanzia tafsiri isiyofaa ya sheria ya Mahakama Kuu yaani; kifungu cha 1 3(1) (a) (b) (c) cha Sheria ya Mawakili Sura ya 341.

Nyingine ni Kanuni ya 4 (1) (a) na (e) ya Kanuni za Mawakili (nidhamu na mashauri mengine), za 2018 GN 120 za 2018 na kuomba maombi hayo yakubaliwe.

Jaji Mashaka amesema kwa mujibu wa maombi  yaliyotupiliwa mbali na waombaji, maombi haya yaliwasilishwa Aprili 3, 2024 ikiwa ni siku tisa baada ya kufutwa kwa maombi ya Machi 25,2024.

“Ni msimamo uliowekwa wa sheria kwamba, pale ambapo hoja ya sheria inayohusika ni haramu au vinginevyo ya uamuzi uliopingwa, hiyo yenyewe inaunda sababu ya kutosha kwa madhumuni ya kuongeza muda ,” amesema.

Jaji Mashaka amesema kwa kuwa waombaji wanataka kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu masuala yanayohusu mamlaka ya mawakili, suala hilo linastahili kuamuliwa na Mahakama.

“Waombaji wameonyesha sababu za kutosha za kuchelewesha kutoa idhini ya kuongeza muda wa kukata rufaa. Hivyo, maombi yamekubaliwa na waombaji wanapaswa kukata rufaa ndani ya siku 60 kuanzia tarehe ya hukumu hii.”

Katika hati ya kiapo cha nyongeza iliyosainiwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Deodatus Nyoni huku mlalamikiwa (Fatma) akiwasilisha hati ya kiapo ya kujibu kupitia wakili wake Peter Kibatala.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo waombaji hao waliwakilishwa na mawakili wawili wa Serikali  ambao ni Erigh Rumisha, Neema Sarakikya, mawakili wa Serikali huku Karume akiwakilishwa na Dk Rugemeleza Nshala na Kibatala.

Wakili Rumisha kupitia hati ya kiapo alieleza kiini cha maombi hayo ni kuongezewa muda wa kukata rufaa.

Katika majibu ya mawakili wa Karume walieleza Deodatus hakuwa na mamlaka ya kuapa hati ya kiapo kwa niaba ya mwombaji wa pili (Kamati ya Mawakili) kwa kuwa hakuruhusiwa kufanya hivyo.

Msingi wa mgogoro

Mgogoro wa uwakili wa Fatma aliyewahi kuwa  Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ulianzia katika mwenendo wa kesi ya Kikatiba  ya mwaka 2018.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Shaibu akipinga kuteuliwa kwa Profesa Adelardus Kilangi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akidai kuwa hakuwa na sifa, lakini Serikali ilimwekea pingamizi la awali.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba, Ado alikuwa akipinga uamuzi wa Rais, hayati John Magufuli aliyekuwa amemteua Profesa Kilangi. Akijibu pingamizi hilo pamoja na mambo mengine Karume alidai kuwa Profesa Kilangi bado ni mchanga kitaaluma, hana uwezo wa kusimamia jukumu alilopewa.

Hivyo Wakili Mkuu wa Serikali aliwasilisha malalamiko Mahakama Kuu, kwamba kauli hizo ni kinyume na kanuni za maadili ya mawakili na ni kejeli na kashfa ya kudhalilisha ofisi ya AG.

Kufuatilia malalamiko hayo, Septemba 20,2019 Jaji Kiongozi, Dk Eliezer Feleshi alimsimamisha Karume kwa muda kutoa huduma za uwakili chini ya kifungu cha 22 (2) (b) cha Sheria ya Mawakili, kusubiri malalamiko dhidi yake kuwasilishwa na kuamuriwa kwenye kamati ya mawakili.

Aidha, alimwelekeza Msajili wa Mahakama Kuu kuwasilisha malalamiko hayo kwenye kamati hiyo.

Karume alifungua shauri la maombi ya mapitio Mahakama ya Rufani akiiomba mahakama hiyo ipitie na kisha kubadili uamuzi wa Mahakama Kuu wa kusimamishwa kwa muda kufanya kazi za uwakili.

Baadaye malalamiko hayo dhidi ya Karume yaliwasilishwa katika Kamati ya Mawakili, kupitia shauri namba la mwaka 2019 badala ya msajili kama ilivyokuwa imeelekezwa na Jaji Feleshi.

Katika shauri hilo aliiomba kamati hiyo imuondoe katika orodha ya mawakili kwa madai ya ukiukaji maadili ya mawakili kutokana na kauli hizo.

Kamati hiyo katika uamuzi wake Septemba 23, 2020 ilimfuta katika orodha ya mawakili baada ya  kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya taaluma hiyo, lakini alikata rufaa Mahakama Kuu Masjala Kuu akipinga uamuzi huo.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na jopo la majaji watatu, Issa Maige (kiongozi wa jopo), Dk Deo Nangela na Edwin Kakolaki ya Juni 21, 2021, ilibatilisha uamuzi wa kamati ya mawakili, kufuatia hoja ya pingamizi la Karume.

Ilisema kuwa kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama, wa Jaji Feleshi, AG hakuwa na haki ya kupeleka malalamiko hayo kwa kamati hiyo isipokuwa msajili, na kwamba kamati hiyo kusikiliza na kuamua shauri hilo ilikuwa inakwenda kinyume na amri ya Jaji Kiongozi.

Serikali haikuridhishwa na hukumu hiyo, hivyo iliomba kibali Mahakama Kuu, ili ikate rufaa, kupinga hukumu hiyo.

Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Stephen Magoiga Desemba 17,2021, iliinyima Serikali kibali cha kukata rufaa kwa kushindwa kuthibitisha kuwepo kesi au hoja zinazopaswa kuamuriwa na Mahakama ya Rufani, ndipo ikafungua maombi haya.

Mahakama ya Rufani katika uamuzi wake wa Juni 27, 2023, uliotolewa na jopo la majaji watatu waliosikiliza shauri hilo, Augustine Mwarija (kiongozi wa jopo) Dk Paul Kihwelo na Mwanaisha Kwariko, ilitupilia mbali shauri la mapitio ya Karume.

Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo kwa kuzingatia hoja moja ya pingamizi la awali la Serikali, kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kumsimamisha Karume uwakili haukupaswa kupingwa Mahakama ya Rufani kwa njia ya mapitio.

Mahakama hiyo imesema kuwa kwa kuwa kifungu cha 22(2) (b) cha Sheria ya Mawakili, ambacho Mahakama Kuu ilikitumia kumsimamisha, pia kinaipa mahakama hiyohiyo mamlaka ya kuondoa amri hiyo ya kusimamishwa wakili kufuatia maombi ya wakili husika.

Kwa mujibu wa uamuzi huo Karume alipaswa kufungua Mahakama Kuu maombi ya kuondolewa amri hiyo ya kusimamishwa badala ya kuchagua kufungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani, uamuzi ambao si sahihi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *