Kesi ya bwana jela anayedaiwa kughushi msamaha wa Rais yakwama tena

Dar es Salaam. Kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili, imekwama kuanza kusikilizwa.

Mkama na wenzake, Sibuti Nyabuya, aliyekuwa ofisa Tehama wa gereza hilo na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, mkazi wa Mbezi, wanakabiliwa na mashtaka  manne yakiwemo ya kughushi msamaha wa Rais kwa wafungwa gerezani na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka hao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hii ni mara ya pili kwa kesi hiyo kushindwa kuanza kusikiliwa kwani Januari 15, 2025 kesi hiyo ilishindwa kuanza usikilizwaji kutokana na hakimu anayesikiliza kesi hiyo Geoffrey Mhini kuwa likizo hivyo kuahirishwa hadi leo.

Hata hivyo, leo Alhamisi, Februari 13, 2025 kesi hiyo ilipangwa kuanza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka, lakini Wakili wa Serikali, Roida Mwakamele aliitaarifu mahakama wakili anayeendesha kesi hiyo yupo kwenye kesi nyingine Mahakama Kuu.

Wakili Mwakamele ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geoffrey Mhini, anayesikiliza shauri hilo.

Amedai kutokana na hali hiyo, anaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi.

Hakimu Mhini amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 13, 2025 itakapoanza kusikilizwa na washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 25517/2024, washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka manne, ambayo ni kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Wanadaiwa kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa ajili ya wafungwa watatu wenye asili ya  China, namba 585/2019 Song Lei; namba 205/2019 Xiu Fu Jie na 206/2016 Haung Quin, waliofungwa katika kesi tofauti kwa makosa ya nyara za Serikali.

Wanadaiwa Desemba 21, 2022, Mkama na Nyabuya walitengeneza nyaraka ya kughushi  yenye kichwa cha habari ‘’Nyongeza ya Msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.

Barua hiyo ya Desemba 21 mwaka 2022,  iliyosainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.

Ingawa wafungwa hao walitekeleza sharti la kulipa Sh45 milioni, hawakuwahi kutolewa gerezani humo, hadi mmoja wao alipotembelewa na Wakili wake akamuonesha barua hiyo, ambayo alipoifuatilia ndipo ikabainika kuwa ni ya kughushi.