Kesi ya Boni Yai, Malisa kuanza kusikilizwa Desemba 19

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Desemba 19, 2024 kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha umma, inayomkabili meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob (42) maarufu Boni Yai.

Mbali na Jacob, mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ya jinai namba 11805/2024 ni Godlisten Malisa (38) ambaye ni ofisa Afya na mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Jacob ambaye ni mkazi wa Mbezi Msakuzi na mwenzake Malisa wanakabiliwa na mashtaka matatu, ambapo mashtaka mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob peke yake.

Washtakiwa hao wameshtakiwa kwa makosa yao, chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Keso hiyo ilipangwa leo Alhamisi, Novemba 21, 2024 kwa ajili ya kuanza usikilizwaji, lakini Hakimu anayesikiliza shauri hilo, Ushindi Swallo yupo likizo.

Wakili wa Serikali, Asiat Mzamiru ameieleza Mahakama hiyo, shauri hilo liliitwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini hakimu anayesikiliza shauri hilo yupo likizo, hivyo anaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Ameahirisha shauri hilo, hakimu Mkazi Mwandamizi, Godgrey Mhini amesema kwa kuwa hakimu anayesikiliza shauri hilo, yupo likizo, kesi hiyo anaiahirisha hadi Desemba 19, 2024 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Washtakiwa wote walikuwepo mahakamani hapo na wanawakilishwa na Wakili Hekima Mwasipu.

Katika kesi ya msingi, Jacob anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya mtandao.

Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kupotosha umma, mshtakiwa alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa X (Twitter) wenye jina la Boniface Jocob@ExMayor Ubungo.

Shtaka la pili ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii linalomkabili Jacob pekee yake.

Mshtakiwa hiyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo mshtakiwa  alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii X ( Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika  kama ifuatavyo.

“MAUAJI ARUSHA, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Shtaka la tatu ni kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee yake, ambapo mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii wa Instagram wenye jina la Malisa_gj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka. 

“Tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi April 2024.

Kwa mara ya kwanza Jacob na Malisa walifikishwa mahakamani hapo Mei 6, 2024 kujibu mashtaka hayo.