
Kigoma. Aliyekuwa msimamizi wa kituo cha kupigia kura katika Mtaa wa Busomero, Kata ya Kasimbu, Manispaa ya Kigoma Ujiji amesema msimamizi wa uchaguzi wa mtaa huo, ambaye alikuwa kiongozi wake, alichokisema mahakamani kuhusiana na fomu za matokeo ya uchaguzi alizomkabidhi siyo kweli.
Msimamizi huyo wa kituo cha kupigia kura Busomero B, Zaki Tegera ameyasema hayo, wakati akihojiwa na Wakili Eliutha Kivyiro, mmoja wa mawakili wa mlalamikaji katika shauri la uchaguzi wa mwenyekiti Mtaa wa Busomero, Kata ya Kasimbu, Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Tegera, Mwalimu wa Shule ya Msingi Azimio, ni shahidi wa tatu wa upande wa walalamikiwa katika shauri hilo alimkana bosi wake huyo, jana Ijumaa Februari 21, 2025, wakati akitoa ushahidi baada ya bosi wake huyo ambaye ni shahidi wa pili kumaliza ushahidi wake.
Shauri hilo limefunguliwa na mwanachama wa ACT- Wazalendo, Khalfan Nyunya, dhidi mwenyekiti wa Mtaa wa Busomero, Hassan Omary, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), aliyetokana na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024.
Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ni aliyekuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa, ambaye ni Ofisa Elimu Kata ya Kasimbu, na msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambaye ni mkurugenzi wa manispaa hiyo.
Nyunya ambaye pia aligombea nafasi ya mwenyekiti wa mtaa huo, katika uchaguzi huo, anapinga mchakato wa uchaguzi na uchaguzi wenyewe uliomuweka Omary madarakani.
Anadai kuwa ni batili kwa kuwa haukuwa huru na wa haki kutokana na kughubikwa na ulaghai na kutokufuatwa kwa kanuni za uchaguzi zilizowekwa.
Anabainisha kasoro zilizojitokeza kuwa ni kuwepo kura bandia zilizowekwa kwenye masanduku ya kura isivyo halali na kufanya tofauti ya idadi za kura zilizopigwa kati nafasi ya mwenyekiti na nafasi ya wajumbe kwa idadi kubwa.
Katika hati yake ya madai na ushahidi alioutoa mahakamani, anaeleza kuwa katika mtaa huo kulikuwa na vituo viwili vya kupigia kura, Busomero A na Busomero B, na kwamba idadi ya wapiga kura katika kituo A kwa nafasi ya mwenyekiti ilikuwa 344.
Kwa nafasi ya wajumbe katika kituo hicho hicho anaeleza kuwa idadi ya waliopiga kura ilikuwa 641, na katika nafasi ya wajumbe viti maalumu walikuwa 437, na kwamba hilo linadhihirisha kuwa kulikuwa na kura zilizowekwa kwenye masanduku isivyo halali.
Katika kituo cha Busomero B, Nyunya anadai kuwa waliopiga kura nafasi ya mwenyekiti walikuwa 369, kwa wajumbe mchanganyiko walikuwa 552 na kwa wajumbe viti maalumu walikiwa 390.
Hivyo, anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa tofauti ya idadi ya kura kati ya nafasi ya mwenyekiti na wajumbe ulisababishwa na kuwepo kwa kura bandia na ibatilishe uchaguzi huo.
Pia, anaiomba mahakama hiyo iwaamuru wajibu maombi wa kwanza na wa pili (msimamizi msaidizi na msimamizi wa uchaguzi) watangaze uchaguzi ndani ya siku saba na ndani ya siku 60 waendesha uchaguzi mpya na wafuate sheria na kanuni.
Katika kuthibitisha madai yake hayo, amewasilisha mahakamani nakala mbili za fomu za matokeo ya mwenyekiti za vituo vyote viwili ambazo zilipokewa na kuwa vielelezo vya ushahidi wake, ambazo alidai kuwa alipewa na msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa.
Kwa upande wake msimamizi huyo msaidizi wa uchaguzi mtaa huo wa Busomero, Ofisa Elimu Kata, wa Kata ya Kasimbu, Mwalimu Jacob Samweli amekana kumpatia mlalamikaji fomu za matokeo na kwamba fomu hizo zilizopokewa mahakamani hazitambui.
Katika ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali, Mzumbe Machunda, shahidi huyo ambaye pia ni mlalamikiwa wa pili, ameieleza mahakama kuwa uchaguzi huo ulifanyika na kumalizika kwa uhuru na haki huku akikana kuwepo kasoro zozote zinazolalamikiwa.
Amedai hapakuwa na utaratibu mgombea kupewa fomu ya matokeo na kwamba fomu za matokeo zilikuwa mbili, moja inabandika na nyingine halisi alikabidhiwa yeye kwa ajili ya kujumlisha kumpata mshindi na baada ya kutangaza matokeo alimkabidhi msimamizi wa uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa).
Hata hivyo, akihojiwa na wakili mwingine wa mlalamikaji, Prosper Maghaibuni anayemwakilisha mlalamiji amekiri kuwa hajawasilisha mahakamani fomu za matokeo ambazo yeye anazitambua.
Alipohojiwa na Wakili Kivyiro amesema kuwa si yeye aliyeandaa na kujaza fomu hizo.
Wakati wa maswali ya kusawazisha majibu ya maswali ya mawakili wa mlalamikaji, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkama Musalama shahidi huyo amedai kuwa fomu za matokeo ya mwenyekiti alizopewa na wasimamizi wa vituo zilikuwa hazijajazwa majina.
Maelezo hayo kuwa fomu alizokabidhiwa na wasimamizi wa vituo hazikuwa zimejazwa majina ya wagombea ndiyo yamepingwa na shahidi huyo wa tatu, msimizi wa kituo, Tegera.
Katika ushahidi wake mkuu wakati akiongozwa na Wakili wa Serikali Fortunatus Mwandu amekana kuwepo kwa kasoro zilizolalamikiwa, akidai kuwa uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki.
Pia, amedai kuwa hazitambui fomu hizo za matokeo ya mwenyekiti na kwamba sio sahihi kuwa wagombea walikuwa wanapewa fomu za matokeo, kwani ziliandaliwa mbili tu, moja ya kubandikwa na nyingine alikabidhiwa msimamizi wa uchaguzi ili kutangaza matokeo.
Alipohojiwa na wakili Ignatus Kaghashe, anayemwakilisha mlalamikiwa wa kwanza, Omary, mwenyekiti anayepingwa, amesema yeye hakuwahi kumpatia Nyunya (mlalamikaji) wala Tigita (shahidi wa pili wa mlalamikaji) fomu za matokeo.
Lakini alipohojiwa na Wakili Kivyiro amekiri kuwa fomu aliyojaza (majina ya wagombea, vyama vyao na kura walizopata) ituoni kwake aligonga mhuri wa duara na aliandika jina lake na kuweka saini, kama inavyoonekana kwenye fomu hizo zilizopokewa mahakamani.
Hivyo, alipoulizwa na Wakili Kivyiro kama msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa (shahidi wa pili, bosi wake) alikuwa mwongo kusema kuwa fomu hizo alizompa hazikuwa zimejazwa majina, amejibu:
“Atakuwa ni mwongo”.
Upande wa utetezi umefunga ushahidi wa upande wake baada ya kuwaita mashahidi wanne na hivyo usikilizwaji wa shauri hilo kwa pande zote umekamilika na Hakimu Kahungu amepanga kutoa hukumu yake Februari 27, 2025