
Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi wa kampuni ya mikopo ya Atlantic Micro Credit Limited, Wendy Ishengoma (38) na wenzake watatu.
Ishengoma na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu, likiwemo la kuendesha biashara ya upatu na kutakatisha fedha Sh3.6 bilioni, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Grace Mwanga ameeleza hayo leo Jumatatu Novemba 11, 2024 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, hivyo kuomba mahakama ipange terehe nyingine.
Hakimu Lyamuya aliahirisha kesi hadi Novemba 26, 2024 itakapotajwa. Kesi hiyo ilisikilizwa kwa njia ya video huku washtakiwa wakiwa rumande.
Mbali na Ishengoma ambaye pia ni mfanyabiashara na mkazi wa Kinondoni, washtakiwa wengine ni Sultan Mdee(29) mhasibu wa kampuni hiyo na mkazi wa Goba; Frank Tengia (34) meneja wa tawi wa kampuni hiyo na mkazi wa Mbezi Juu pamoja na Mwiga Mwiga(31) ambaye ni ofisa masoko wa kampuni hiyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 Jijini Dar es Salaam, kwa makusudi waliongoza na kusimamia genge la uhalifu kwa kufanya biashara ya upatu.
Shtaka la pili ni kuendesha biashara ya upatu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Januari 18, 2024 na Oktoba 11, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa katika kipindi hicho walifanikiwa kuendesha biashara ya upatu kwa kutoa ahadi kwa wanachama na kuingia mikataba ya ubia yenye thamani ya Sh3.63 bilioni kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Shtaka la tatu ni kutakatisha fedha, ambapo washtakiwa wanadaiwa katika kipindi hicho ndani ya Jiji la Dar es Salaam, walijipatia Sh 3.63 bilioni wakati wakijua kuwa wanapokea fedha hizo ni mazao ya kosa tangulizi la jinai ambalo ni kuendesha biashara ya upatu.