Kesi mbili za ‘Boni Yai’ na Malisa kuunguruma leo, moja ikitajwa 

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Februari 12, 2025  inatarajia kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha umma, inayomkabili Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob(42) maarufu Boni Yai.

Jacob ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani na mwenzake Godlisten Malisa (38) na mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, wanakabiliwa na kesi ya Jinai namba 11805/2024 ni Godlisten Malisa (38) na mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mwanasiasa huyo na Malisa wanakabiliwa na mashtaka matatu, ambapo mashtaka mawili kati ya hayo yamkabili Jacob peke yake.

Kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Kesi ya msingi:

Washtakiwa hao wameshtakiwa makosa yao, chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jacob anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kinyume na kifungu cha 16 cha sheria ya mtandao.

Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo April 22, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kupotosha umma, mshtakiwa  alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa X (Twitter) wenye jina la Boniface Jocob@ExMayor Ubungo.

Shtaka la pili ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii linalomkabili Jacob pekee yake.

Mshtakiwa hiyo anadaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo mshtakiwa  alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii X ( Twitter) wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika  kama ifuatavyo.

“MAUAJI ARUSHA, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.

Shtaka la tatu ni kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee yake, ambapo mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Malisa anadaiwa siku hiyo ya tukio, kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa Kijamii wa Instagram wenye jina la Malisa_gj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka” tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi Aprili 2024.

Wakati huo huo, kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob pekee yake, itatajwa katika mahakama hiyo.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapishaji taarifa za uwongo kwenye mtandao wake wa X (zamani Twitter).

Kesi hiyo ya jinai inasikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Boni Yai anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.

Katika shtaka la kwanza, Boni anadaiwa Septemba 12, 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uwongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar Es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).

Taarifa hizo zinasomeka kuwa:

“Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”

Katika shtaka la pili, mshtakiwa anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo kuwa zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.

Ujumbe huo inasomeka kuwa:

“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu …, bali Ma-RCO waliokuwa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, 2024 kujibu mashtaka yanayomkabili.