Kesi kuporomoka jengo Kariakoo yaendelea kupigwa kalenda

Dar es Salaam. Upande wa mashitaka umedai bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kuua bila kukusudia inayowakabili watu sita wakiwemo wamiliki wa jengo lililoporomoka Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne Mei 13, 2025, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ambao wote ni wafanyabiashara na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni Leondela Mdete (49), mkazi wa Mbezi Beach, Zenabu Islam (61), mkazi wa Kariakoo na Ashour Awadh Ashour (38), mkazi wa Ilala.

Wengine ni Soster Nziku (55), mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe (59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku (28) mkazi wa Mbezi beach.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji iliyopo mahakamani hapo.

Kamala ameieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geodfrey Mhini, kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.

“Mheshimiwa hakimu, washtakiwa wote wapo mbele ya Mahakama yako na kesi yao imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa, lakini upelelezi wake bado unaendelea, hivyo tunaomba Mahakama itupangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema Kamala.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 12, 2025 itakapotajwa na washtakiwa wote wapo nje kwa dhamana.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.

Katika shitaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusababisha kifo cha Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.

Vile vile, wanadaiwa kusababisha kifo cha  Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.

Pia, wanadaiwa isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *