
Kigoma. Mahakama ya Wilaya ya Kigoma imekataa kupokea fomu za matokeo ya uchaguzi wa wajumbe wa Mtaa wa Busomero, Kata ya Kasimbu iliyopo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kuwa kielelezo cha ushahidi katika shauri la uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa huo kutokana na mkanganyiko wa jina la shahidi.
Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo jana Ijumaa, Februari 21, 2025 baada ya kukubaliana na hoja moja ya pingamizi la mawakili wa Serikali kutokana na tofauti ya herufi moja ya jina la shahidi linalosomeka katika fomu hiyo na jinsi alivyolitaja mahakamani.
Jina hilo lililoibua mgogoro ni Hamis katika matamshi lakini katika maandishi kwa mujibu wa shahidi mwenye jina lake linaanza na herufi K badala ya H, hivyo linaandikwa Khamis badala ya Hamis.
Wakati kimaandishi kwa mujibu wa shahidi linaanza na herufi K, lakini lilivyoandikwa katika fomu hizo ambazo shahidi huyo aliomba Mahakama izipokee linaanza na H.
Hivyo, kukosekana au kutokuanza na heruki K katika maandishi kwenye fomu hizo ndiko kulikoifanya Mahakama izikatae fomu hizo.
Jinsi ilivyokuwa
Mwanachama wa ACT Wazalendo, Khalfan Nyunya amefungua shauri la uchaguzi dhidi mwenyekiti wa Mtaa wa Busomero, Hassan Omary, wa Chama cha Mapinduzi (CCM), aliyetokana na uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024.
Walalamikiwa wengine katika shauri hilo ni aliyekuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa, ambaye ni Ofisa Elimu Kata ya Kasimbu na msimamizi wa uchaguzi Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambaye ni mkurugenzi wa manispaa hiyo.
Nyunya ambaye pia aligombea nafasi ya mwenyekiti wa mtaa huo, katika anapinga mchakato wa uchaguzi na uchaguzi wenyewe uliomuweka madarakani Omary kama mwenyekiti wa mtaa huo.
Anadai kuwa ni batili kwa kuwa haukuwa huru na wa haki kutokana na kughubikwa na ulaghai na kutokufuatwa kwa kanuni za uchaguzi zilizowekwa.
Anabainisha kasoro zilizojitokeza kuwa ni kuwepo kura bandia zilizowekwa kwenye masanduku ya kura isivyo halali na kufanya tofauti ya idadi za kura zilizopigwa kati nafasi ya mwenyekiti na nafasi ya wajumbe kwa idadi kubwa.
Anaeleza kuwa katika mtaa huo kulikuwa na vituo viwili vya kupigia kura, Busomero A na Busomero B, na kwamba katika hali ya kushangaza idadi ya wapiga kura katika kituo A kwa nafasi ya mwenyekiti ilikuwa 344.
Kwa nafasi ya wajumbe katika kituo hicho hicho anaeleza kuwa idadi ya waliopiga kura ilikuwa 641, na katika nafasi ya wajumbe viti maalumu walikuwa 437, na kwamba hilo linadhihirisha kuwa kulikuwa na kura zilizowekwa kwenye masanduku isivyo halali.
Katika kituo cha Busomero B, Nyunya anadai kuwa waliopiga kura nafasi ya mwenyekiti walikuwa 369, kwa wajumbe mchanganyiko walikuwa 552 na kwa wajumbe viti maalumu walikiwa 390.
Hivyo anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa tofauti ya idadi ya kura kati ya nafasi ya mwenyekiti na wajumbe ulisababishwa na kuwepo kwa kura bandia na ibatilishe uchaguzi huo.
Pia anaiomba mahakama hiyo iwaamuru mjibu maombi wa kwanza na wa pili (msimamizi msaidizi na msimamizi wa uchaguzi watangaze uchaguzi ndani ya siku 7 na ndani ya siku 60 waendesha uchaguzi mpya na wafuate Sheria na kanuni.
Katika kuthibitisha madai yake hayo, pamoja na maelezo ya ushahidi wake wa mdomo aliouwasilisha mahakamani, pia amewasilisha nakala mbili za fomu za matokeo ya mwenyekiti za vituo vyote viwili ambazo zilipokewa na kuwa vielelezo vya ushahidi wake.
Japo mawakili wa Serikali walimwekea pingamizi lakini mawakili wake, Eliutha Kivyiro na Prosper Maghaibuni walipangua hoja zote baada ya mahakama katika uamuzi wake kukubaliana na hoja zao na kulitupilia mbali pingamizi hilo kuwa halina mashiko.
Nyunya baada ya kuhitimisha ushahidi wake, ndipo akamuita shahidi wake huyo.
Shahidi huyo amejitambulisha kwa majina matatu kuwa anaitwa Mussa Khamis Tigita, huku akimsisitizia Hakimu Anna Kahungu anayesikiliza shauri hilo kuwa jina lake hilo la katikati linaanza na K na H.
Kisha akiongozwa na Wakili Maghaibuni ameieleza mahakama kuwa katika uchaguzi huo aligombea wa nafasi wa ujumbe wa mtaa huo na kwamba katika mtaa huo kulikuwa na vituo viwili vya kura, Busomero A alipata kura 64 na Busomero B alikopata kura 78.
Amesema alifahamu kuwa alipata kura hizo baada ya kupewa fomu ya matokeo na msimamizi wa kituo na akaiomba mahakama hiyo izipokee fomu hizo mbili za matokeo ya nafasi ya ujumbe ya vituo vyote viwili ziwe vielelezo vya ushahidi katika shauri hilo.
Fomu hizo zinaonesha idadi ya waliopiga kura kwa kila kituo ndizo zilikusudiwa kuunga mkono madai ya tofauti ya idadi wa waliopiga kura kwa nafasi ya mwenyekiti na kwa nafasi ya wajumbe kwa kuoanisha na fomu za matokeo ya mwenyekiti zilizopokelewa mahakamani.
Mawakili wa Serikali wakiongozwa na kiongozi wa jopo hilo, Mkama Musalama baada ya kuzikagua ndipo wakaibua pingamizi Mahakama isizipokee.
Wamebainisha sababu mbalimbali ikiwemo hiyo ya tofauti ya herufi ya jina lake la kati baina ya lililoandikwa kwenye fomu na jinsi yeye alivyoielekeza Mahakama linavyoandikwa.
Katika sababu hiyo, Wakili Musalama amesema kuwa shahidi huyo hana uhusiano na hizo fomu kwani jina la katikati lililoko kwenye fomu hizo limmeanza na herufi H (Hamis) wakati shahidi katika maelezo yake amesema kuwa jina lake linaanza na herufi K (Khamis).
Hivyo, Wakili Musalama amesema jina lililoko kwenye fomu hizo ni la mtu mwingine kabisa tofauti na shahidi huyo (kutokana na tofauti ya herufi hiyo moja, japo jina la kwanza na la mwisho yanafanana).
Hivyo, amesema kuwa shahidi huyo si shahidi anayestahili kutoa mahakamani fomu hizo kuwa kielelezo katika shauri hilo.
Mawakili wa mlalamikaji walipinga hoja zote za pingamizi hilo wakidai kuwa hazina mashiko ya kisheria huku wakidai kuwa tofauti ya herufi moja katika jina la katikati ni kasoro ndogo isivyo na athari kulingana na msingi aliouweka shahidi kabla ya kuomba fomu hizo zipokewa.
Hakimu Kahungu katika uamuzi wake ametupilia mbali hoja nyingine zote za pingamizi hilo kuwa hazina mashiko, lakini akasema tatizo analiona kwenye jina la shahidi.
“Tatizo naliona kwenye jina. Wakati nachukua maelezo nilikuwa nimeacha kuanza na K katika jina lake la Khamis lakini mwenyewe akasisitiza kuwa linaanza na K. Kwa hiyo, ninaona kuwa nyaraka hii haihusiani na shahidi huyu,” amesema Hakimu Kahungu na kuhitimisha:
“Hivyo ninaiona hii kama ni kasoro ambayo inakwenda kwenye mzizi wa suala na kwa sababu hiyo ninakubaliana na pingamizi hili na nyaraka zinazokusudiwa kutolewa kama kielelezo zinakataliwa.”