Kenya yaunga mkono msimamo wa Tanzania kuwazuia kina Martha Karua

Kenya yaunga mkono msimamo wa Tanzania kuwazuia kina Martha Karua

Dar/Nairobi. Waziri Kiongozi wa Baraza la Mawaziri la Kenya, Musalia Mudavadi ameiunga mkono kauli ya Rais Samia Suluhu kuhusiana na wanaharakati wa mataifa ya nje kuingilia mambo ya Tanzania.

Akizungumza leo Jumatano Mei 21, 2025, kwenye mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha Citizen cha Kenya, Mudavadi amesema kauli ya Rais Samia ni sahihi huku akidokeza kuwa baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakitumia vibaya uhuru uliopo nchini humo.

Kauli ya Mudavadi imetolewa kufuatia mwanasiasa wa Kenya, Martha Karua na Jaji Mkuu wa zamani wa Kenya, Willy Mutunga kuzuiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JKIA) na kisha kurudishwa kwao.

Wakenya hao walikuja nchini Tanzania kwenye kesi ya uhaini na kuchapisha taarifa za uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu. Kesi hiyo iliyosikilizwa juzi na kuahirishwa hadi Juni 2, 2025.

“Sitaipinga [Kauli ya Rais Samia] kwa sababu nadhani kuna ukweli ndani yake. Tuangalie hoja kadhaa. Kiwango cha adabu, matusi tunayoyaona Kenya, pamoja na kuwa tuna uhuru wa maoni, kuna wakati kuna kuvuka mipaka,” Mudavadi anaeleza akijibu swali la mwandishi, Yvonne Okwara.

Okwara alihoji iwapo Serikali ya Kenya ina mpango wa kuchukua hatua za kulalamika kidiplomasia hasa juu ya hoja ya ‘watovu wa adabu’.

“Rais Samia amesema watu wanavuka mipaka (katika kutoa maoni), huo ni ukweli. Mimi ni Mkenya pia, ukweli ni kuwa; namna tunavyofanya mambo na tunavyoongea, kwa sababu kuna uhuru wa maoni, hakuna heshima,” Mudavadi amemjibu mwandishi huyo.

Akizungumza Mei 19, 2025 wakati akizindua Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Rais Samia alionya juu ya wanaharakati kutoka nje wanaongilia mambo ya Tanzania, wengi wakihusisha kauli hiyo na wanaharakati aliofika Tanzania kufuatilia kesi ya Lissu wakitokea nchini Kenya.

“Tumeanza kuona mtiririko wa wanaharakati ndani ya kanda yetu hii, kuanza kuvamia na kuingilia mambo yetu. Sasa kama kwao wamedhibitiwa, wasije kutuharibia huku. Tusitoe nafasi, walishaharibu kwao, walishavuruga kwao, nchi iliyobaki haijaharibika, watu wanaishi kwa amani na usalama ni hapa kwetu,” alisisitiza Rais Samia.

Rais Samia aliongeza: “Niwaombe sana vyombo vya ulinzi na usalama na Wizara ya Mambo ya Nje, kutotoa nafasi kwa watovu wa adabu wa nchi nyingine kuja kufanya vurugu hapa. Hapana. Nimeiona clip kadhaa za kunisema, kwamba niko bias, ninachofanya ni kulinda nchi yangu. Kwa hiyo hatutatoa nafasi kwa kiumbe yoyote, awe wa ndani au nje ya nchi.”

Kauli ya Mudavadi imepigiliwa msumari na Msemaji wa Serikali ya Kenya, Isaac Mwaura ambaye amesema Tanzania imetekeleza wajibu wake kwa kuzingatia uhuru wake kwa kuwazuia watu kadhaa wa wakiwemo wanasiasa na wanaharakati wa Kenya, wakiongozwa na Martha Karua na kwamba Kenya haiwajibiki katika uamuzi huo.

“Ikiwa Serikali ya moja ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itaamua kumkataa mtu binafsi kuingia nchini mwao, ina mamlaka ya kufanya hivyo,” amesema Mwaura.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Kenya inaheshimu uhuru wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na haiingilii uamuzi wao wa ndani.

“lkiwa wameamua hivyo, huo ni uamuzi wao. Hatujui kwa nini watamzuia mtu, na Serikali ya Kenya haihusiki,” amesema msemaji huyo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *