Hatimaye Profesa Kithure Kindiki ameapishwa kuwa Naibu Rais mpya wa Rais wa Kenya, kuja kurithi mikoba ya Rigathi Gachagua ambaye alibanduliwa mamlakani na Bunge la nchi hiyo mwezi uliopita wa Oktoba.
Katika hafla hiyo ya aina yake iliyofanyika katika Jumba la Mikutano la KICC jijini Nairobi, Kindiki ameapishwa na Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama, Winfrida Mokaya, huku Jaji Mkuu Martha Koome akishuhudia.
Rais William Ruto amehudhuria tukio hilo la kihistoria, akiwaongoza Wakenya kumkaribisha Kindiki kama Naibu Rais wa tatu wa nchi hiyo chini ya Katiba mpya 2010.
Kindiki akiwa ameandamana na mke wake, Dkt. Joyce Kithure, amekula viapo viwili, kiapo cha utii na kiapo cha afisi, akitangaza kujitolea kwake kuwahudumia wananchi wote wa Kenya bila ubaguzi na upendeleo.
Akilihutibua taifa baada ya kula kiapo, Kindiki amesema, “Nimekuwa mwanafunzi wako mwema kwa miaka 20. Nimejifunza kuwa mnyenyekevu na mwaminifu, sitakuangusha katika majukumu mapya uliyonitwika.”

Profesa Kindiki ambaye hadi anachukua wadhifa huu mpya alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Usalama wa Taifa ameapishwa siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Kenya kutupilia mbali kesi za zilizowasilishwa na mawakili wa Gachagua kupinga kuapishwa kwa Kindiki.
Gachagua alitimuliwa na Bunge la Seneti la Kenya mwezi uliopita kwa mashtaka matano kati ya 11 yaliyowasilisihwa dhidi yake, yakiwemo kuchochea migawanyiko ya kikabila na kuhujumu Idara ya Mahakama.