Kenya imekiri kwamba ilisaidia katika utekaji wa mwanasiasa wa upinzani wa Uganda katika ardhi yake mwaka uliopita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kizza Besigye, 68, alitekwa nyara na watu ambao walikuwa wamejihami kwa silaha jijini Nairobi mwezi Novemba mwaka wa 2024 kabla yake kuonekana katika mahakama ya kijeshi nchini Uganda siku chache baadaye.
Besigye daktari wa zamani wa rais Yoweri Museveni, ambaye ameongoza Uganda kwa karibia miaka 40, amekuwa akijaribu kuwania katika uchaguzi wa urais dhidi ya Museveni bila mafanikio.
Awali serikali ya Kenya ilikuwa imekanusha kuhusika katika utekaji wa mwanasiasa huyo mkongwe.

Akizungumza katika mahojiano na Televisheni ta ndani, Waziri wa mambo ya kigeni wa Kenya, Musalia Mudavadi alikiri kwamba nchi yake ilishirikiana na mamlaka ya Uganda kwenye suala hilo.
“(Uganda) ni nchi rafiki. Yeye (Kizza Besigye) hakuwa anaomba hifadhi hapa. Hakuwa amekuja kusema kwamba alikuwa anaomba hifadhi. Kama angesema hivyo labda angeshugulikiwa kwa namna nyengine tofauti,” Mudavadi aliambia runinga ya Citizen.
“Tunahitaji kushirikiana na mataifa wanachama wa EAC na kwa wakati mwegine tunahitajika kushugulikia ushirikiano huo vyema kwa ajili ya manufaa ya kitaifa,” aliongeza.
Mashirika ya kutetea haki za bindamu yanasema mashtaka ya uhaini dhidi ya Besigye yanahusishwa na uchaguzi mkuu wa mwezi Januari.
Inatarajiwa kwamba huenda Museveni mwenye umri wa miaka 80 atakuwa anatafuta kuchaguliwa tena kwa muhula mwengine.
Kesi dhidi ya Besigye ilihamishiwa katika mahakama ya kiraia baada yake kuanza mgomo wa kutokula chakula mapema mwaka huu.

Baada ya kesi yake kusikilizwa siku ya Jumatano ya wiki hii ilihairishwa hadi Mei 29.
Wanaharakati wanasema hatua za serikali kuwateka wanachama wake na kuwafungulia mashtaka ni sehemu ya njama ya serikali kuyumbisha demokrasia barani Afrika.
Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania Tundu Lissu naye pia anakabiliwa na kesi ya uhaini kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.