Kenya yakana kuhusika na kutekwa nyara Kizza Besigye

Serikali ya Kenya imekana kuhusika na madai ya kutekwa nyara kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni nchini Kenya, Sing’oei Korir, amesema, Kenya haina jukumu lolote katika madai ya kukamatwa au kufukuzwa kiongozi huyo mkongwe wa upinzani nchini Uganda.

“Hakuna sababu yoyote kwa Kenya kuwa mshiriki katika kukamatwa kwake,’’ Korir alisema.

Besigye ameshindana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika chaguzi nne na kushindwa mara zote, ingawa amekuwa akipinga matokeo ya chaguzi hizo.

Siku ya Jumatano, mke wa Besigye, Winnie Byanyima, alidai mumewe alikuwa ametekwa nyara jijini Nairobi siku ya Jumamosi katika jumba moja katika eneo la Riverside Drive.

Kulingana na familia yake, Besigye alitekwa nyara jijini Nairobi na kupelekwa Uganda, ambako wanajeshi wanadaiwa kumzuilia.

Wakati huo huo, Kizza Besigye, mwanasiasa mkongwe nchini Uganda leo amefikishwa katika Mahakama ya Kijeshi ya Makindye, nchini Uganda.

Yeye na mwenzake, Obedi Lutale, wamekanushwa mashtaka yanayowakabili.

Amerejeshwa rumande hadi Desemba 2.

Mahakama ya Kijeshi nchini Uganda inamshtaki Besigye kwa makosa manne ikiwemo kupatikana na silaha katika hoteli moja jijini Nairobi.