Kenya yachunguza kifo cha mtu aliyekufa kituo cha polisi

Kifo hicho kimezusha shutuma kutoka kwa wafuasi na shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International. Kifo cha Albert Ojwang kilijiri wiki chache kabla ya kumbukumbu ya machafuko mabaya yaliyotokea katika maandamano ya kupinga kupandishwa kodi na ufisadi. Maandamano hayo yalisababisha ukandamizaji mkali wa serikali ya Rais William Ruto dhidi ya wakosoaji.

Polisi ilisema katika taarifa kuwa Ojwang alikamatwa kwa kuchapisha habari ya uwongo na akapata majeraha kichwani baada ya kugonga kichwa chake kwenye ukuta wa chumba alichokuwemo katika kituo cha polisi jijini Nairobi.

Taarifa hiyo imesema maafisa wa polisi waliokuwa zamu waligundua majeraha hayo mara moja na kumkimbiza katika hospitali ya Mbagathi, ambapo alitangazwa kuwa tayari alikuwa amefariki. Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi – IPOA imeanzisha uchunguzi kuhusu tukio hilo. Amnesty International imesema kifo cha Ojwang akiwa kizuizini siku ya Jumamosi lazima kichunguzwe haraka, kwa kina na kwa njia huru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *