
Nchi ya Kenya na Umoja wa Ulaya, zimekubaliana kuendelea kushirikiana kibiashara chini ya mkataba wa EPA, ambapo suala la kuhuisha teknolojia kama ya akili mnemba na teknolojia nyingine kwenye biashara limepigiwa chapuo.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Mwaka 2023 Kenya na umoja wa Ulaya zilitiliana saini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara, ambapo sasa bidhaa za kenya isipokuwa silaha zimepewa ahueni ya ushuru kwenye soko la Ulaya.
Akizungumza katika kongamano la pili la jukwaa la kibiashara kati ya kenya na umoja wa Ulaya, mkuu wa ujumbe wa Ulaya nchini Kenya, Henriette Geiger, ametoa wito wa kuhuisha biashara na teknolojia.
“Ubunifu umebadili kabisa namna tunafanya biashara, na unatoa fursa za kipekee kuimarisha zaidi ushirikiano wetu kiuchumi. Chinik ya mpango mkakati wa EU, umoja wa Ulaya uko tayari kuwekeza katika ubora wa miundombinu na uungwanishwaji wa intanet”. Alisema Henriette Geiger
Kwa upande wake waziri viwanda, biashara na uwekezaji wa Kenya, Lee Kinyanjui, amesifu ushirikiano na umoja wa Ulaya, akisema kenya imeendelea kufaidika kiuchumi.
“Tunatambua mchango wa umoja wa Ulaya wa kuwa mshirika mkubwa wa biashara na maendeleo wa Kenya. Tunatoa wito kwa makampuni zaidi ya Ulaya kuja kuwekeza Kenya. Na uwepo wenu leo hii unatoa nafasi ya kipekee kwa biashara za kati na kubwa za Ulaya zinazotafuta fursa mpya kuwekeza Kenya na Afrika kwa ujumla. ” Alieleza Lee Kinyanjui.
Aidha rais wa Kenya, William Ruto, mbali na kutaka ushirikiano huu kuboreshwa, amesisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji akiahidi serikali yake kuunda sera rafiki za kibiashara.
“Tumejidhatiti kuhakikisha tunatekeleza sera nzuri za kibiashara, ambazo sio tu zitakuza ushirikishaji katika kutengeneza utajiri lakini kutoa fursa zaidi. Lengo letu ni kujenga uchumi imara na stahimilivu ambao utamnufaisha kila mkenya. Lazima twende mbele zaidi ya kuwa na nia njema, ili kuleta matokeo chanya kwa biashara zetu, wawekezaji na raia wa kawaida. ” Alieleza rais Ruto
Kwa mujibu wa takwimu za umoja wa Ulaya, niashara kati ya Kenya na EU ilifikia kiasi cha Euro bilioni 3.4 mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 mwaka uliotangulia, na asilimia 53 katika kipindi cha miaka 10.