
Nchini Kenya, ukarabati wa viwanja kadhaa vya soka unamtia wasiwasi Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Katika ripoti yake ya hivi punde, iliyochapishwa wiki hii, Nancy Gathungu ananyooshea kidole dosari ambazo zinahusu hasa miundombinu ya mji mkuu, Nairobi. Hali ya wasiwasi, kwani Kenya inatazamiwa kuwa mwenyeji, pamoja na Tanzania na Uganda, wa michuano ya CHAN mwezi Agosti na AFCON mwaka ujao.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Nairobi, Gaëlle Laleix
Huu ni upotevu halisi wa pesa ambao Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anafichua katika ripoti yake ya hivi punde. Inahusu viwanja kadhaa maarufu jijini Nairobi, kama vile uwanja wa zamani wa City, ambao sasa umepewa jina la uwanja wa Joe Kadenge. Uwanja huu haujaandaa mashindano makubwa kwa takriban miaka kumi.
Ukarabati wake ulizinduliwa mnamo mwezi Agosti 2023, lakini mwaka mmoja na nusu baadaye, mradi huo umesimama, kulingana na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Mjenzi alitelekeza mradi, baada ya kupokea nusu ya gharama zilizotumika, yaani shilingi milioni 41 (zaidi ya euro 290,000).
Uwanja wenye mteremko na mashimo…
Suala lingine linalotia wasiwasi ni uwanja wa Dandora. Ukarabati wake umegharimu shilingi milioni 223 za Kenya, zaidi ya euro milioni 1.5. Licha ya hayo, Mkaguzi Mkuu aligundua taa zenye hitilafu, hakuna mfumo wa taa wa ndani na uwanja wenye mteremko na mashimo ndani yake.
Viwanja viwili vikubwa vitakavyoandaa mashindano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) havijatajwa kwenye ripoti hiyo. Lakini Kenya ilikuwa imeahidi uboreshaji wa jumla wa miundombinu yake, ikiwa ni pamoja na viwanja vya mafunzo. Mnamo mwezi wa Januari, CAF ilitangaza kuahirisha michuano ya CHAN kutoka mwezi Februari hadi mwezi Agosti 2025, kutokana na ukosefu wa miundombinu inayokidhi viwango vya kimataifa.