
Mzozo unaendelea kutanda nchini Kenya kufuatia kifo cha Albert Ojwang, aliyekamatwa Jumamosi, Juni 7, 2025, kufuatia malalamishi kutoka kwa kamanda wa pili wa polisi, ambaye alimshutumu kwa kumharibia jina kwenye mitandao ya kijamii. Albert Ojwang alifariki saa chache baada ya kukamatwa. Inadaiwa aligonga kichwa chake ukutani katika chumba ambako alikuwa anazuiliwa, kulingana na polisi. Toleo hili rasmi limetiliwa shaka.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu huko Nairobi, Albane Thirouard
Uchunguzi wa maiti ya Albert Ojwang ulipangwa kufanyika siku ya Jumatatu. Uliahirishwa na hatimaye umepangwa kufanyika leo Jumanne. Baba yake alisubiri saa kadhaa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti. Matokeo yanasubiriwa kwa hamu, kwani toleo la polisi kwa tukio hilo linatiliwa shaka, na kuibua maswali kadhaa.
Kama Julius Juma, wakili wa familia, akieleza kwa waandishi wa habari: “Bado hatujajua sababu kamili ya kifo cha Albert, na ni nani anayehusika. Ikiwa alikamatwa kwa sababu zilizotajwa hapa, kwa nini aliwekwa kwenye kifungo cha upweke? Kwa nini tunaambiwa aligonga kichwa chake ukutani? Mwili wake ulikuwa na majeraha mengi: kichwani, mikononi, mabegani. Kichwa chake kimevimba kabisa.”
Wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu pia walifika katika chumba cha kuhifadhia maiti kudai haki kwa Albert Ojwang. Hussein Khalid, mkuu wa Vocal Africa, shirika la kutetea haki za binadamu, alifanya siku nzima huko: “Tunasema: inatosha. Tumepoteza watu wengi sana ambao walikuwa mikononi mwa polisi. Kwa mazingira yoyote yale, hakuna mtu anayefaa kufariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi.”
Polisi wanashikilia kuwa Albert Ojwang alipatikana akiwa amepoteza fahamu katika chumba alikokuwa aakizuiliwa. Baada ya hapo alipelekwa hospitali ambapo alitangazwa kuwa amefariki baada ya kufika hospitalini. Maafisa wote waliokuwepo usiku huo wamesimamishwa kazi ili kuwezesha uchunguzi. Idara ya polisi imetangaza kuwa imeanza uchunguzi wake.