KenGold yajishtukia, yaipiga mkwara Azam

SARE tatu mfululizo ilizopata KenGold katika mechi za Ligi Kuu Bara, zimemshtua kocha wa timu hiyo, Omar Kapilima na kusema ameshakaa na wachezaji na kuwaambia kwa hali yoyote ni lazima wapate ushindi mbele ya Azam FC ili kurejesha morali ya kuondoka eneo la mkiani mwa msimamo.

KenGold imebakiza mechi saba za kuamua hatma ya kubaki Ligi Kuu au kurudi Ligi ya Championship, kati ya hizo nne ni za nyumbani na tatu za ugenini huku rekodi kwa ujumla kwa timu hizo zikiwa hazivutii tangu ipande daraja msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kapilima alisema licha ya kikosi hicho kuwa na mabadiliko makubwa kiuchezaji, mtihani mkubwa uliopo ni kushindwa kung’oka nafasi ya mwisho katika msimamo kitendo ambacho kisaikolojia kinawavunja moyo wachezaji na benchi kwa ujumla.

“Bado tuna nafasi kubwa ya kucheza ligi msimu ujao kama tutaweza kupata matokeo ya pointi tatu katika mechi mbili au tatu mfululizo tukianza na Azam nyumbani, hii naamini itarudisha nguvu kwa wachezaji kwani tunaweza kusogea,” alisema Kapilima ambaye ni kocha msaidizi na kuongeza;

“Ni kweli hatuna rekodi nzuri nyumbani wala ugenini, lakini hilo haliwezi kuondoa sisi kupata matokeo na kubaki kucheza msimu ujao, kinachonipa jeuri ni namna wachezahji wangu wanavyopambana na kuonyesha ubora iwe ugenini na nyumbani.”

Kapilima amezungumza hayo wakati kikosi hicho kikiburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 16 baada ya kushinda michezo mitatu kati ya 23 iliyocheza. Imepoteza michezo 13 na sare saba.

Nyumbani KenGold imeshinda mechi tatu, imepoteza tatu na sare tano wakati ugenini haijashinda hata mchezo mmoja zaidi ya kupata sare mbili na kupokea vipigo 10.

Kwa sasa KenGold inajiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam utakaochezwa Aprili 4 mwaka huu kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Kapilima aliongeza, licha ya muda mchache aliokuwa nao ila atahakikisha wanapambana kutengeneza eneo la ulinzi baada ya kuteseka na washambuliaji ambapo sasa wanafunga mabao ila changamoto mpya imekuwa ni eneo la ulinzi ambako wanaruhusu mabao mengi.

Kocha huyo aliyefundisha na kucheza timu mbalimbali hapa nchini zikiwamo Majimaji, Yanga na Mtibwa Sugar, alijiunga na kikosi hicho Oktoba 22 mwaka jana akichukua nafasi ya Fikiri Elias aliyeamua kuondoka mwenyewe Septemba 17, mwaka jana.

Fikiri aliondoka kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo ambapo aliiongoza katika michezo mitatu tu ya Ligi Kuu Bara na kati yake alipoteza yote akianza kufungwa 3-1 dhidi ya Singida Black Stars, Fountain Gate (2-1) kisha KMC (1-0).