KenGold wajipa matumaini Ligi Kuu Bara

WAKATI Kocha Mkuu wa Ken Gold, Omari Kapilima akituliza presha kwa mashabiki, timu hiyo haishuki daraja, habari njema ni baadhi ya mastaa waliokuwa nje kwa changamoto mbalimbali huenda wakarejea kikosini.

Ken Gold iliyopanda Ligi Kuu msimu huu haijawa na matokeo mazuri ikiwa inaburuza mkia na pointi 16 ikibakiwa na mechi sita tu kumaliza msimu na kusubiri hatma yake.

Katika mechi zilizobaki itacheza ugenini tatu ikianza na Dodoma Jiji Aprili 6, Coastal Union na Namungo ya kuhitimishia msimu, huku nyumbani ikiwa ni dhidi ya Prisons, Pamba na Simba kisha kusubiri hatma yake.

Hata hivyo, pamoja na usajili iliyokuwa imefanya dirisha dogo, wapo baadhi ya nyota wa kigeni ambao hawajacheza hata dakika moja, wakisubumbuliwa na majeraha na kukosa vibali.

Habari njema ni kuwa mastaa, Benard Morison aliyekuwa majeruhi amerejea vyema, huku mdogo wake Ernest Morison kibali naye freshi na wanasubiri uamuzi wa benchi la ufundi.

Pia wamo Erick Kabamba raia wa Congo ambaye naye amerejea kikosini huku uongozi ukipambania vibali kwa mastaa Mubashid Seidu (Ghana) na Abdul Abdulai kutoka Nigeria.

Ofisa Habari wa timu hiyo, Jose Mkoko alisema wachezaji hao muda wowote huenda wakaonekana uwanjani kutegemeana na mahitaji ya timu kwa kuwa baadhi wako tayari, huku wengine mipango ikiendelea.

“Wengine ni maamuzi ya kocha akiona wanahitajika kulingana na mechi husika watacheza, wengine uongozi unaendelea na mchakato wa haraka kukamilisha leseni na vibali waingie uwanjani,” alisema Mkoko.

Kwa upande wake Kocha Kapilima alisema pamoja na matokeo wanayopitia kwa sasa, lakini mechi sita zilizobaki ni za kufia uwanjani kuhakikisha timu inabaki salama Ligi Kuu.

Alisema kwa sasa wanaenda kujipanga upya kusahihisha makosa ikiwamo eneo la beki ambalo kila mchezo wameruhusu bao kurekebisha makosa na kuboresha maeneo mengine kufanya kweli.

“Tunakwenda kuwasha moto dhidi ya Dodoma Jiji, makosa yaliyoonekana tutayafanyia kazi, niwatoe hofu mashabiki, timu haishuki daraja, dakika 540 zinatosha kutuacha salama Ligi Kuu,” lisema Kapilima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *