
WAKATI KenGold na Mashujaa zikishuka uwanjani leo, makocha wa timu hizo wamepiga hesabu kali kila mmoja akisisitiza pointi tatu muhimu.
Timu hizo zinakutana rekodi ikiwabeba Mashujaa baada ya mechi ya duru la kwanza kushinda mabao 3-0 nyumbani Uwanja wa Lake Tanganyika, mkoani Kigoma.
Mchezo huo utakaopigwa leo Jumatano kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Mashujaa inaingia uwanjani ikiwa haijapata ushindi katika mechi mbili zilizopita za ligi na kushika nafasi ya 11 kwa pointi 23 baada ya michezo 22.
Mashujaa mara ya mwisho kushinda katika ligi iliichapa Pamba Jiji 2-0 nyumbani, kisha ikafungwa 5-0 na Yanga na kupokea kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Singida Black Stars kabla ya leo kukabiliana na KenGold.
Kichapo cha mabao 3-0 ilichokipata Mashujaa kutoka kwa Singida Black Stars, ndicho kilihitimisha safari ya kocha Bares kuiongoza timu hiyo.
KenGold ambayo ipo mkiani mwa msimamo wa ligi ikikusanya pointi 15, imeonyesha mabadiliko makubwa duru la pili baada ya kushinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza moja dhidi ya Yanga kwa mabao 6-1.
Kocha msaidizi wa Mashujaa, Charles Fred alisema ikiwa mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu tangu kukabidhiwa jukumu hilo, anahitaji kuanza upya kupata ushindi na kurejesha furaha kikosini.
“Mechi itakuwa ngumu na tutawaheshimu wapinzani, lakini tunaenda kuanza upya, vijana wako tayari kwa mechi hiyo na matarajio ni kushinda ili kurudisha morali kikosini,” alisema Fred aliyechukua nafasi ya Abdalah Mohamed ‘Bares’ ambaye Februari 26, 2025 alivunjiwa mkataba.
Kocha msaidizi wa KenGold, Omary Kapilima alisema licha ya kuendelea kumkosa staa wao, Bernard Morison, lakini hesabu zao ni kushinda ili kufufua matumaini ya kubaki salama Ligi Kuu.
Alisema baada ya kufululiza sare katika mechi tatu, leo kazi itakuwa ni kupambania pointi tatu ambazo zitawaweka katika mazingira mazuri ya kujiondoa nafasi ya mkiani waliyopo hivi sasa.
“Morison alikuwa majeruhi, kwa sasa anaendelea na mazoezi mepesi, tunasubiri ripoti ya daktari, kwa jumla tuko fiti kupambania alama tatu ili kujiweka pazuri,” alisema Kapilima.
Morison hajacheza mchezo wowote kati ya sita ambayo timu hiyo imecheza tangu asajiliwe dirisha dogo na awali ilielezwa vibali vyake havijawa tayari na huenda angeanza dhidi ya Mashujaa leo.
KenGold imebakiza mechi nane kuamua hatma yake katika ligi ikiwa ni msimu wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara.
Katika mechi hizo nane zilizoshikilia hatma yao, safari inaanza leo dhidi ya Mashujaa (nyumbani), Azam (nyumbani), Dodoma Jiji (ugenini), Tanzania Prisons (nyumbani), Coastal Unionn (ugenini), Pamba Jiji (nyumbani), Simba (nyumbani) na Namungo (ugenini).
Inachofanya KenGold ambayo maboresho yake kipindi cha dirisha dogo yameonekana kuwabeba ni kuhakikisha inajiondoa mkiani mwa msimamo.
Timu hiyo yenye maskani yake jijini Mbeya, ilishuhudiwa duru la kwanza ikikusanya pointi sita pekee baada ya kucheza mechi 15, lakini duru la pili katika mechi saba imekusanya tisa.
Mashujaa nayo haipo salama sana kwani nafasi ya 11 na pointi zake 23, tofauti yake na mstari wa kushuka daraja ni pointi saba pekee, hivyo inahitaji kushinda kutengeneza nafasi ya kujiweka salama.