LIGI Kuu Bara inaendelea kupigwa tena leo kwa michezo mitatu katika viwanja na mikoa mbalimbali na itaanzia jijini Mbeya na Dar es Salaam kwa mechi za 10:00 jioni, huku saa 1:00 usiku ikichezwa mchezo mmoja makao makuu ya nchi Dodoma.
Kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, KenGold iliyotoka sare ya bao 1-1, ugenini mechi ya mwisho mjini Tabora dhidi ya Tabora United, itaikaribisha Kagera Sugar, yenye kumbukumbu nzuri baada ya mchezo wa mwisho kuifunga Fountain Gate mabao 3-0.
Timu zote zinakutana zikiwa hazina ubora katika maeneo yote mawili kwa maana ya safu ya ulinzi na ushambuliaji na KenGold imefunga mabao 15 na kuruhusu 36, huku kwa upande wa Kagera Sugar ikifunga 16 na nyavu zake zikitikiswa mara 27.
Ushindi kwa KenGold utaamsha angalau morali ya kuendelea kupigania kutoshuka daraja, ingawa hata kama ikishinda itasalia mkiani na pointi 13, kwani kwa sasa ina 10, huku Kagera ikiwa itashinda itasogea hadi nafasi ya 14 kutoka iliyopo ya 15.
KenGold itaendelea kumtegemea nyota wa timu hiyo, Selemani Bwenzi mwenye mabao matatu hadi sasa, akiwa katika kiwango bora kwenye michezo aliyocheza, baada ya kufunga mfululizo kuanzia mchezo na Yanga, Fountain Gate na Tabora United FC.
Kwa upande wa Kagera Sugar inategemea ubora wa nyota wa kikosi hicho raia wa Uganda, Peter Lwasa anayeongoza kwa kufunga mabao ambapo hadi sasa amefunga saba, huku Salehe Kambenga akifunga mawili akionyesha pia kiwango kizuri kikosini humo.
Kocha msaidizi wa KenGold, Omary Kapilima alisema pointi nne walizopata katika michezo miwili zimewapa morali wachezaji ya kupambana, huku akieleza wanaangalia uwezekano wa kuziba nafasi ya kiungo, Zawadi Mauya aliyeonyeshwa kadi nyekundu.

“Mauya atakosekana baada ya kadi nyekundu aliyoipata mchezo wetu wa mwisho na Tabora United, tutaangalia namna nzuri ya kuziba pengo lake kutokana na wachezaji waliopo, hatupo nafasi nzuri hivyo ni lazima tucheze kwa nidhamu kubwa.”
Kwa upande wa Kocha wa Kagera Sugar, Melis Medo alisema licha ya ushindi mchezo wa mwisho na Fountain Gate ila bado ana kazi kubwa ya kufanya, kwani michezo mingi wamekuwa hawana mwenendo mzuri ugenini, ingawa imeongeza hali ya kujiamini.
Mchezo huu utakuwa wa kisasi kwa KenGold, kwani mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba Septemba 20, mwaka jana ilikubali kichapo cha mabao 2-0, ambayo yote yalifungwa na Mganda Peter Lwasa dakika ya 1 na 65.

Mchezo mwingine wa Saa 10:00, jioni utapigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex jijini Dar es Salaam na wenyeji KMC FC, baada ya kuchapwa na Yanga mabao 6-1, itajiuliza kwa Maafande wa JKT Tanzania waliochapwa 1-0 na Singida Black Stars.
KMC inaingia katika mchezo huo ikiwa haina safu nzuri ya ulinzi na ya ushambuliaji, kwani hadi sasa imefunga mabao 14, ikiwa ya tatu kwa kufunga machache, baada ya Tanzania Prisons (9), huku JKT Tanzania na Pamba FC kila moja ikifunga 11.
JKT Tanzania iliyovunjiwa rekodi yake ya kutopoteza mchezo ikiwa nyumbani dhidi ya Singida Black Stars ilipochapwa bao 1-0, imecheza michezo minane bila ya kuonja ushindi tangu ilipoifunga Fountain Gate bao 1-0, Novemba 29, mwaka jana.

Katika michezo hiyo, JKT imechapwa minne na kutoka sare minne, ikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara saba, jambo linalosubiriwa kuona ni kwa jinsi gani kikosi hiki cha maafande kitabadilisha upepo mbaya iliokuwa nao.
Kocha wa KMC, Kally Ongala alisema baada ya kipigo cha mabao 6-1, dhidi ya Yanga, alikaa na wachezaji na kuwajenga zaidi kisaikolojia, huku akiwataka kusahau yaliyopita na kuangalia mchezo huo, anaoutumia kurejesha hali ya kujiamini tena.
Kwa upande wa Kocha wa JKT Tanzania, Ahmad Ally alisema changamoto kubwa iliyopo ni ufinyu wa kikosi hicho katika baadhi ya nafasi ingawa anaendelea kupambana na hali iliyopo, huku akiweka wazi hawapotezi kwa sababu pia ya kucheza tu vibaya.
Mara ya mwisho timu hizi zilipokutana zilitoka suluhu Septemba 22, mwaka jana, huku michezo miwili ya Ligi Kuu iliyopita kukiwa hakuna mbabe, japo KMC iliifunga JKT Tanzania ilipokuwa ndio mwenyeji, ilipoichapa mabao 2-1, Septemba 15, 2023.
KMC iliyopo nafasi ya saba na pointi 22, ikiwa itashinda itasogea hadi ya sita na kuishusha Coastal Union yenye pointi 22 pia, zikitofautiana kwa mabao, huku JKT iliyopo nafasi ya 12, endapo itashinda itasogea hadi ya saba na pointi 23.
Mchezo wa mwisho leo, utapigwa saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo wenyeji, Dodoma Jiji iliyotoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Namungo, itaikaribisha maafande wa Tanzania Prisons, waliotoka kuchapwa michezo miwili mfululizo.

Dodoma Jiji haijaonja ladha ya ushindi katika michezo miwili mfululizo tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mashujaa mabao 3-1, Desemba 28, mwaka jana na kati ya hiyo imepoteza mmoja kwa bao 1-0, mbele ya Pamba na sare ya 2-2 na Namungo.
Dodoma iliyocheza michezo 18, ikishinda mitano, sare mitano na kupoteza minane na kukusanya pointi 20, ikiwa itashinda mchezo huo inaweza kusogea hadi nafasi ya sita kutoka ya 13 iliyopo, ikitegemeana na tofauti ya mabao na wapinzani wake.
Kwa upande wa Prisons, inashika nafasi ya 14 na pointi 17, baada ya kucheza michezo 19, ikishinda minne, sare mitano na kupoteza 10, ikiwa timu pekee kati ya 16 za Ligi Kuu, zenye safu butu ya ushambuliaji baada ya kufunga mabao tisa tu.
Mbali na Prisons kuandamwa na safu butu ya ushambuliaji hadi sasa kutokana na kufunga idadi ndogo ya mabao kati ya timu 16 za Ligi Kuu Bara, pia imekuwa haina rekodi nzuri ugenini na katika michezo tisa iliyocheza haijashinda hata mmoja.
Katika michezo hiyo tisa iliyocheza ugenini msimu huu katika Ligi Kuu Bara, Prisons imepoteza mitano na kutoka pia sare minne, huku mchezo wa mzunguko wa kwanza zilipokutana jijini Mbeya, timu hizo zilitoka suluhu (0-0), Septemba 21, mwaka jana.
Wakizungumzia mchezo huo, Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime alisema anaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wao ila muhimu ni kupata pointi tatu nyumbani, huku Amani Josiah wa Prisons akieleza wamefanyia kazi mapungufu hususani eneo la ulinzi.