
Ken Gold imeshindwa kujinasua mkiani baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Mashujaa, huku mashabiki wa timu hiyo wakionekana kuvurugwa na matokeo hayo.
Baada ya mchezo kumalizika, mashabiki walijikusanya katika geti kubwa wakionyesha kutofurahishwa na matokeo hayo hadi Polisi walipowatawanya.
Katika mchezo huo ambao umepigwa Uwanja wa Sokoine, Ken Gold ilionekana kuwa na matumaini makubwa kushinda, lakini hadi dakika 90 zinaisha, timu zote ziligawana alama moja.
Mashujaa ndio walitangulia kupata bao la mapema kupitia kwa Jafari Kibaya, kabla ya kujifunga kupitia Yusuph Dunia na kudumu hadi mapumziko, huku kila upande ukionesha ushindani na nia ya alama tatu.
Kipindi cha pili timu zote zilizonyesha soka safi huku Ken Gold wakitengeneza nafasi kadhaa, lakini wakishindwa kuzitumia vyema kabla ya dakika ya 46 Mishamo Daud kujipatia bao la pili kwa mpira wa faulo uliopigwa na Sele Bwenzi.
Mashujaa hawakukata tamaa na kufanya shambulizi lililowapa bao la kusawazisha kupitia kwa Ally Nasor ‘Ufudu’ na kufanya dakika 90 kuisha kwa matokeo hayo.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Charles Fred amesema sare hiyo siyo matokeo mabaya akipongeza kiwango cha nyota wake kuwa anauona mwanga mzuri katika mechi zijazo baada ya kukabidhiwa majukumu kuiongoza timu hiyo.
“Mechi ilikuwa ngumu lakini vijana wamepambana na kuweza kusawazisha hadi kuondoka na pointi moja, kwetu siyo mbaya na nimeridhishwa na kiwango cha wachezaji,” amesema Fred.
Kocha wa Ken Gold, Omary Kapilima walihitaji ushindi lakini makosa yaliyoonekana wanaenda kusahihisha kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya Azam akitoa matumaini kwa mashabiki kuwa wasikate tamaa.
“Zimebaki mechi saba, makosa yaliyoonekana leo tutaenda kusahihisha ili mechi zijazo tuweze kufanya vizuri, mashabiki wasikate tamaa bado tunayo nafasi,” amesema Kapilima.