
KAMATI ya waamuzi nchini imefanya mabadiliko ya mwamuzi wa kati wa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Tabora United na Simba.
Katika mchezo huo unaochezwa leo Februari 2, awali mwamuzi wa kati alipangwa kuchezesha, Amina Kyando kutoka Morogoro, lakini baada ya muda mfupi amepigwa chini na nafasi yake kuchuliwa na Kefa Kyombo wa Mbeya kwa ajili ya mechi hiyo.
Kyando aliyepangwa kusaidiana na Robert Luhemeja na Fatma Mambo, tangu uteuzi wake ufanyike amekuwa katika presha kubwa juu ya mchezo huo unaopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, kutokana na matukio tata aliyoamua mbele ya wenyeji hao.
Kwenye mechi mbili ambazo Kyando ameziamua za Tabora United dhidi ya Biashara United iliyopigwa Juni 12,2024 alitoa penalti iliyozusha utata wakati wa mchezo wa kuamua timu ipi ipande Ligi Kuu Bara au kubaki Championship msimu uliopita.
Penalti hiyo iliyotolewa dakika ya 90+7 kati ya dakika 9 za nyongeza ndio iliamua mchezo huo ambapo hata hivyo kwenye mchezo wa marudiano Tabora iliibuka na ushindi ulioibakisha Ligi Kuu Bara.
Mchezo mwingine ulikuwa dhidi ya Simba msimu uliopita wa kumalizia msimu, ambapo Kyando alikataa bao halali la Tabora United lililofungwa kwa shuti kali na aliyekuwa kiungo wa kikosi hicho, Najim Mussa, na badala ya kuweka mpira kati aliiacha Simba ianzishe shambulizi la haraka lililoenda kuzaa bao la kuongoza la Wekundu wa Msimbazi wakati Tabora wakiendelea kudai bao walilonyimwa.
Hata hivyo, mchezo huo uliofanyika Mei 6, 2024 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Simba ilishinda mabao 2-0, yaliyosababisha baadaye mwamuzi huyo kufungiwa.
Timu hizo zinakutana huku Simba ikiwa na kumbukumbu ya kushinda mchezo wa kwanza msimu huu jijini Dar es Salaam mabao 3-0, Agosti 18, mwaka jana.