Keane ahofia kiwango Man United

Manchester, England. Kiwango cha Manchester United katika mechi ya raundi ya nne ya Kombe la FA kimempa wasiwasi nyota wa zamani wa timu hiyo, Roy Keane licha ya ushindi wa mabao 2-1 nyumbani ambao iliupata dhidi ya Leicester City na kusonga mbele hadi raundi ya tano.

Licha ya ushindi wa Manchester United wa mabao 2-1 kwenye raundi ya nne ya Kombe la FA dhidi ya Leicester City, kiungo wa zamani wa timu hiyo, Roy Keane amewataka mashabiki wasipumbazike na matokeo hayo kwani bado haichezi vyema.

Keane alisema kuwa ushindi ulificha udhaifu mkubwa ambao Manchester United ilionyesha mbele ya Leicester City hivyo mashabiki hawapaswi kuamini kuwa timu yao imeshakaa kwenye mstari hivi sasa.

“Sielewi, hakuna nishati, tunaenda na mbinu ni lazima ucheze ukiwa na nishati. Ndio pointi ya kuanzia. Haijalishi ni mfumo gani ambao unaucheza, hauwezi kumsogelea yeyote. Unatakiwa ukabe watu wawili. Tumeziona timu mbili mbaya (Manchester United na Leicester City).

“Msiwe wapumbavu, mnapaswa kuwapongeza kwa kuingia raundi ya tano lakini kiwango chenyewe hakikaribia kuwa katika ubora,” alisema Keane.

Keane alisema kuwa namna Manchester United inavyocheza hivi sasa, haiendani na hadhi ya klabu hiyo.

“Kwa sasa wanakwaza sana. Wanatakiwa kuwakumbusha wachezaji katika vyumba vya kubadilishia nguo, mechi inahusu nini. Hakuna nishati kwa wachezaji na uwanjani. Wanasubiria kwa kitu kutokea.

“Kukosekana kwa hali ya kujiamini, wanapoteza mipira kirahisi. Ninajaribu kulitazama hili kwa muono wa United,” alisema Keane.

Katika mchezo wa juzi, Manchester United ambayo ilitanguliwa kufungwa bao katika kipindi cha pili, ilizitumia vyema dakika 45 za pili kupata mabao mawili kupitia kwa Joshua Zirkzee na Harry Maguire huku lile la kufutia machozi la Leicester City likipachikwa na Bobby Reid.

Hata hivyo bao la Maguire limegeuka mjadala kwani picha za marudio ya video zimeonyesha kuwa beki huyo alikuwa ameotea wakati alipofunga.

Pengine bao hilo lingekataliwa ikiwa teknolojia ya usaidizi wa video kwa marefa (VAR) ingekuwa inatumika katika mechi hiyo kwani haikuwepo.