Kazi iliyo mbele ya mwenyekiti mpya wa AUC

Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Youssouf, anakabiliwa na changamoto lukuki zinazolikabili Bara la Afrika kwa sasa, ikiwemo mapigano Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na kukatwa kwa misaada inayotolewa na Serikali ya Marekani kwa Afrika.

Youssouf, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti, ameshinda kinyang’anyiro cha uenyekiti wa AUC kilichokuwa na ushindani mkali dhidi ya Waziri Mkuu mstaafu wa Kenya, Raila Odinga, wakitofautiana kwa kura 11 katika duru ya saba ya upigaji kura.

Hii ilikuwa wakati wa Mkutano wa 38 wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia, uliofanyika huku kukiwa na vita katika eneo la Mashariki mwa DRC ambapo waasi wa M23 wanapigana na jeshi la taifa hilo (FARDC).

Hata hivyo, Odinga alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho katika awamu ya sita baada ya kuzoa kura 22 dhidi ya 26 za Youssouf.

Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, Richard Randriamandrato, pia alikuwa katika kinyang’anyiro hicho ambacho kilishuhudia jumla ya nchi 49 zikipiga kura kuchukua nafasi ya Moussa Faki Mahamat wa Chad, ambaye amemaliza muda wake.

Youssouf alisema muda mfupi baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tano wa AUC kwamba “ameheshimiwa sana,” na kuwashukuru Odinga na Randriamandrato kwa “kujitolea na maono” yao.

“Pamoja, tutafanya kazi kuelekea Afrika iliyoungana na yenye ustawi. Ninaahidi kuhudumu kwa uadilifu na kujitolea kwa ajili ya kuboresha bara letu,” alisema kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii wa X.

Mwenyekiti wa AUC atahudumu kwa muhula wa miaka minne, na ataweza kugombea tena kwa muhula wa pili pekee.

Mwenyekiti atafanya kazi kama Ofisa Mtendaji Mkuu, mwakilishi wa kisheria wa AU na Ofisa Mkuu wa Uhasibu wa Tume.

Majukumu ya Mwenyekiti ni pamoja na wajibu wa jumla wa usimamizi wa fedha za Tume, kukuza na kutangaza malengo ya AU na kuimarisha utendaji wake, kushauriana na kuratibu na wadau wakuu kama vile nchi wanachama na washirika wa maendeleo, miongoni mwa wengine.

Jukumu hilo pia linajumuisha kuteua na kusimamia wafanyakazi wa AUC na kufanya kazi kama msimamizi wa mikataba na mambo ya kisheria ya AU.

Utekelezaji wa Ajenda 2063 ya AU unakabiliwa na changamoto huku baadhi ya malengo yakiwa tayari hayajafikiwa. Afrika ina wasiwasi hasa kuhusu kupoteza mikataba ya kimataifa kama vile mikataba ya ushirikiano wa kiuchumi, ubia wa kimkakati wa biashara na uwekezaji, na hata sheria nzuri ya zamani ya fursa ya ukuaji wa Afrika (Agoa).

Rais wa Marekani, Donald Trump, anapoathiri mabadiliko haya wakati akitekeleza ajenda yake ya ‘Marekani Kwanza,’ kuna hofu kwamba washirika wengine wa Magharibi wanaweza kufuata mkondo huo.

Agoa, ambayo imewezesha nchi zinazostahiki za Kiafrika kusafirisha baadhi ya mazao yao kwenda Marekani bila kulipa ushuru tangu mwaka 2000, itakuwa chanzo kikuu cha wasiwasi kwa AUC kwani haijabainika iwapo Trump atairejesha upya.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Dk Salim Ahmed Salim, Denis Konga, anasema Youssouf anakabiliwa na changamoto nyingi mbele yake, kubwa ikiwa vita katika eneo la Maziwa Makuu, hususan waasi wa M23 huko DRC na nchi kunyoosheana vidole.

Anasema viongozi wa Afrika wamekuwa wakialikwa na mataifa makubwa, jambo ambalo linapishana na Mkataba wa Banjul, ambao walikubaliana kwamba watakuwa wakituma wawakilishi.

“Viongozi wa Bara la Afrika wamekuwa wakiongoza kukimbilia kwenye mikutano ya mataifa makubwa duniani. Kwa hiyo, utaona, labda yeye ataweza kusimamia hilo kama ni sehemu ya mamlaka yake, kuhakikisha kwamba tunarudi kwenye misingi ya kurudisha heshima ya Afrika,” amesema.

Ameongeza kwamba AU isionekane ni klabu ya wazee, isiwe ni klabu ya marais kukutana kunywa kahawa, bali iwe ni sehemu ambayo inaweza kusimamia maazimio yaliyopo, na yeye (Youssouf) kama kiongozi wa sekretarieti anapaswa kusimamia maazimio hayo.

Kuhusu suala la Agoa, Konga amesema ilikuwa inatoa unafuu zaidi kwa Wamarekani kwa sababu Waafrika walikuwa wanapeleka bidhaa Marekani ambazo zinaratibiwa na Wamarekani wenyewe, kwa maana ya bidhaa wanazozitaka wao na bei pia wanapanga wao.

“Ifike sehemu wao wawe wanakuja kutuomba sisi, kwamba tunaomba hiki, sio wanatengeneza utaratibu ambao unaleta unafuu kwao halafu sisi tunashangilia kwa sababu sehemu ndogo ya watu wanapata faida,” anasema.