Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemvaa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira huku kikisisitiza tangu nchi ipate uhuru hakuna kilichofanyika.
Kauli hiyo ya Chadema ni muendelezo wa majibizano kati ya Chadema na Wasira ambaye hivi karibuni alijibu mashambulizi ya chama hicho akisema CCM imefanya mambo makubwa ya kimaendeleo.
Januari 18, 2025, Wasira alichaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM kuwa Makamu mwenyekiti amefanya ziara Geita, Dar es Salaam, Mara na jana Jumanne, alimaliza ziara yake mkoani Mwanza.

Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Lamadi Mkoa wa Simiyu leo Jumatano Februari 12, 2025 akiwa njiani kwenda Tarime.
Katika maeneo hayo, Wasira amekuwa wakitupa ‘vijembe’ kwa Chadema kwamba wamemaliza uchaguzi wao wakiwa mafungu mafungu baada ya Tundu Lissu kuibuka mshindi wa uenyekiti dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa anatetea nafasi hiyo.
Januari 3, 2025, Wasira akiwa Bunda Mjini alisema kutokana na maendeleo waliyoleta ikiwemo ujenzi wa miundombinu kinajivunia na hakina mpango wa kuondoka madarakani kwa sasa.
“Nashangaa watu wanaohoji CCM imefanya nini kipindi cha miaka 60 ya uhuru, kipindi tunapata uhuru tulikuwa na barabara tatu tu zote zilikuwa zinatumiwa na wazungu kwenda mashamba ya mikonge na kahawa kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro, kutoka Tanga kwenda Korogwe na kutoka Moshi kwenda Arusha,” nakuongeza
“Hivi sasa Serikali ya CCM, imeunganisha nchi nzima kwa barabara za lami leo unaweza kutoka hapa kwa usafiri wa bajaji hadi mkoa wa Mtwara,” alisema.
Leo Jumatano, Februari 12, 2025, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amerejea nyumbani kwao mkoani Mara akianza kufanya mkutano Lamadi, Mkoa wa Mara kisha akaenda Bunda Mjini alipozaliwa Wasira, pamoja na Tarime Mjini.
Hoja ya CCM haijafanya chochote, imetolewa mkoani Simiyu na Heche na wanachama na viongozi wengine wakisema Wasira mwenye miaka 80 anahitaji kupumzika.
Heche katika maelezo yake amesema licha ya nchi kuwa na utajiri mkubwa wa raslimali kama madini, utalii na ardhi lakini chama kilichopo madarakani kimeshindwa kuzitumia kwa ufanisi ili kuboresha maisha ya wananchi wake.

Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Lamadi Mkoa wa Simiyu leo Jumatano Februari 12, 2025 akiwa njiani kwenda Tarime.
“Leo nchi hii ina miaka 63 baada ya kupata uhuru hakuna cha maana kilichofanyika, kula ni tatizo, maji ya kunywa ni tatizo katika nchi hii, mwanamke akipata mimba na kwenda kujifungua hata mume wake anaaza kupata mimba ya mawazo,” amesema Heche.
Heche amesema chama hicho hiyo siyo nchi wanayotaka kwani kutoka Tarime, Geita hadi Singida ni dhahabu na Kaskazini kuna mlima mkubwa wa Kilimanjaro, kuna mbuga kubwa na kuna maziwa makubwa.
“Mungu ametupendelea Tanzania ni nchi ambayo wananchi wake walitakiwa kutoa misaada kwenye nchi nzingine lakini watu wetu kula ni tatizo na tukisema watu waende mbinguni kiingilio Sh20,000 wote mtashindwa na kwenda motoni,” amesema.
Amesema Tanzania imefanywa kuwa maskini kutokana na aina ya viongozi wanaoitawala, nchi mawazo yao yamechoka hawana fikra mpya na hao watu kesho atatoka Wasira lakini baada ya muda fulani anarudi tena.
“Tuna viongozi wa aina ileile tangu uhuru, Wasira kwanza ni mzee na kusinzia mara kwa mara ni haki yake, alichafanya kazi kubwa kwanza alikuwa mkuu wa mkoa na kwa umri wake hajielewi hawezi kujua matatizo ya wananchi hasa vijana wenye umri mdogo,” amesema.
Heche amewataka wananchi na makada wa chama hicho kukiunga mkono chama hicho kwa kuhakikisha wanaondoa mfumo huo na kurudisha mamlaka kwa wananchi, huku akieleza wajipanga kufanya mabadiliko na hawaogopi.
Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini akiwa Bunda Mjini amerejea maelezo hayo na kuwaomba wananchi kuwaunga mkono yeye na Lissu kwenye kuwaongoza katika kupigania rasilimali za nchi.
“Hatima ya kuondoa matatizo yetu iko mikononi mwetu wananchi. Kama wewe ni maskini, unaweza kuamua mtoto wako arithi umaskini huo au abadilishiwe maisha na kupata elimu bora,” amesema Heche.
Heche amehimiza mshikamano wa wananchi katika kupigania mabadiliko, akisisitiza kuwa Chadema iko tayari kushirikiana na Watanzania wote kuhakikisha mamlaka yanarudi kwa wananchi.
Jumamosi Februari 8, 2025 katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya Tarime mkoani Mara, Wasira alisema kwa miaka 60 iliyopita Watanzania wamekuwa na hali bora zaidi kimaisha.
“Unasimama unasema hatujafanya kitu, tumefanya, tumesomesha watu wengi sana hata wanaosema hatujafanya chochote tumewasomesha na uhuru wa kusema hatujafanya chochote tumewapa,” amesema Wasira.

Makamu Mwenyekiti Chadema, John Heche wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Lamadi Mkoa wa Simiyu leo Jumatano Februari 12, 2025 akiwa njiani kwenda Tarime.
Katika msisitizo wake, Wasira alisema: “Wako wengine wanasema miaka 60 eti hatujafanya kitu, naomba muwasamehe kwa kuwa hawajui wanachosema, kwa sababu mimi kwa umri wangu nilikuwepo niliijua Tarime kabla ya uhuru na nawaona wapo wazee hapa pia waliijua.”
‘Tuungane kuondoa CCM’
Awali, katika mapokezi hayo Lamadi, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila alizungumzia mambo mawili, jambo la kwanza Katiba ya Tanzania Ibara ya 8, inasema msingi wa mamlaka ya nchi ni wananchi.
“Taifa letu kwa sheria tulizonazo, taratibu za uchaguzi zinasema msingi wa mamlaka yeyote katika taifa hili ni watu wanaitwa watendaji wa vijiji, kata, wakurugenzi na watu wa Tume ya Uchaguzi wao wanaamua nani awe kiongozi na nani hapaswi kuwa kiongozi,” amesema.
Mahinyila amesema kutokana na hali hiyo, vijana na makada wa chama hicho wasikubali kufuata mfumo huo kwa kushiriki uchaguzi ambao baadhi ya watu wanaenda kuwachagulia mtu wa kuwa kiongozi.
“Shughuli hiyo hatutaifanya siku ya uchaguzi nyie vijana wa Lamadi, na sehemu nyingine nafikiri Mwenyekiti wetu atatoa msimamo leo, vijana wa Chadema hatutakuwa tayari kupangiwa viongozi na baadhi ya watu,” amesema.
Mahinyila alizungumzia jambo la pili ni changamoto zinazowakumba vijana mathalani ajira na kupotea, huku akiwataka wasinyamaze bali wanapaswa kupaza sauti vinginevyo wote watapotezwa.
Naye aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Patrick Ole Sosopi akizungumza kwenye mapokezi Bunda Mjini amewaomba wananchi kukubali kufanya mabadiliko kwani CCM imeshindwa kuyabadili maisha ya wananchi wake licha ya utitiri wa raslimali.