Mwanza. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akitangaza nyongeza ya kima cha chini cha mshahara cha asilimia 35.1 kwa watumishi wa umma, baadhi ya wananchi na watumishi wa sekta ya umma wameelezea matokeo ya uamuzi huo.
Rais Samia alitangaza kiwango kipya cha mshahara wa kima cha chini kwa watumishi wa umma, jana Alhamisi, Mei Mosi, 2025, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mkoani Singida, huku akiwataka watumishi wa sekta binafsi kuondoa hofu kwani suala lao linafanyiwa kazi.
Kutokana na nyongeza hiyo itakayoanza Julai mwaka huu, kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma sasa kitakuwa Sh500,000 kutoka Sh370,000 iliyokuwa ikilipwa kabla ya makato ya kodi.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Mei 2, 2025, Mhandisi Mshauri wa Mradi wa Daraja la Kigongo–Busisi, Abdulkarim Majuto amesema uamuzi huo utaongeza motisha wa kufanya kazi kwa watumishi wa sekta ya umma.
Majuto amesema anaamini kuwa kutokana na ongezeko hilo la mshahara kwao, litasaidia kupunguza changamoto lukuki, ikiwemo uchukuaji wa mikopo umiza uliokuwa ukifanywa na watumishi wa umma kwa kisingizio cha mshahara kutotosheleza.
“Hii fedha iliyoongezwa tunaamini kwamba itasaidia watumishi kupangilia vizuri bajeti zao na kutumia kiasi cha nyongeza katika shughuli na mahitaji ya ziada. Kwa hiyo naamini angalau hata bajeti za watumishi zitaongezeka,” amesema Majuto.
Mkazi wa Nyegezi, Mwanza, Otto Rwegasira amesema uamuzi huo wa Rais Samia utaongeza ufanisi kwa watumishi kwa kile alichodai wengine walikuwa wakitoroka kazini mapema kwenda kufanya shughuli za kuwazalishia kipato cha ziada.
Rwegasira amesema zawadi pekee ambayo watumishi wa umma wanaweza kumpatia Rais Samia ni kufanya kazi kwa weledi, kuongeza juhudi katika kazi na kuhudumia umma kwa moyo mkunjufu.
“Kutokana na mshahara kiduchu, watumishi wa umma wamekuwa wakitoroka kazini kwenda kufanya kazi nyingine, ili kutengeneza kipato cha ziada kukidhi mahitaji kwenye maisha ambayo gharama zimepanda juu,” amesema Rwegasira.

Kwa upande wake, Mkazi wa Kilimanjaro, Rashid Rashid amesema ongezeko hilo la mshahara kwa walimu limerejesha tumaini na ari ya ufanyaji kazi, na anaamini kuwa uchumi wa nchi utaimarika.
“Ongezeko hili la mshahara limetupa matumaini mapya kama walimu. Tunajisikia kuthaminiwa na tuko tayari kuongeza ufanisi kazini,” amesema Rashid.
Mwanaima Saleh, Mkazi wa Moshi Mjini, mkoani humo, amesema kuwa ongezeko la mshahara litaongeza weledi katika kazi, na wafanyakazi wataongeza bidii na kujituma zaidi.
“Hili ongezeko linatupa sababu ya kufanya kazi kwa moyo mmoja. Bila shaka tutakuwa na tija zaidi kwenye maeneo yetu ya kazi,” amesema Mwanaima.
Kauli ya Saleh inaungwa mkono na Mkazi wa Tabata, Dar es Salaam, Saidi Salehe ambaye amesema uamuzi huo umepokelewa vizuri na utasaidia kuleta morali kwa wafanyakazi wa umma kujituma zaidi.
“Nimelipokea vizuri tena kwa furaha, na zaidi ni kumpongeza rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kuliona na kutupa ongezeko hilo. Nawashauri watumishi wenzangu tufanye kazi kwa bidii ili tuweze kuitia moyo Serikali yetu,” amesema.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiwa na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson pamoja na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Tumaini Nyamhokya wakiimba Wimbo wa Mshikamano (Solidarity Forever) kwenye Maadhimisho ya Siku wa Wafanyakazi Duniani Mei Mosi ambapo Kitaifa Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Bombadia Mkoani Singida tarehe Mei 1, 2025.
Kwa upande wake, mamalishe katika Stendi ya Mabasi Shinyanga, Ghati Nyaki amesema anaamini kupitia ongezeko hilo la kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma, hata biashara yake itaongezeka kutokana na mzunguko wa fedha kuongezeka.
“Kwa kawaida mtu akilipwa mshahara mzuri hata matumizi yake yanaongezeka, kwa hiyo naamini kupitia hilo hata sisi tulioko kwenye mnyororo huu tutakuwa tumenufaika maana watakuwa wakitumia fedha zao,” amesema Nyaki.
(Imeandikwa na Mgongo Kaitira – Mwanza, Ombeni Daniel – Kilimanjaro, Ally Mlanzi – Dar es Salaam na Hellen Mdinda – Shinyanga).