
Dar es Salaam. Wadau na wanazuoni nchini wameshauri Jeshi la Polisi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutafuta suluhu kwa njia ya mazungumzo.
Wameeleza hayo baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano ya Chadema jana Septemba 23, 2024, huku likiwakamata baadhi ya viongozi na wafuasi wa chama hicho.
Chadema ilipanga kufanya maandamano iliyoyaita ya maombolezo na amani kupinga matukio ya utekaji na mauaji nchini, yakiwamo ya makada wake.
Wadau hao pia wameitaka Serikali itimize wajibu wake wa kulinda usalama wa raia na kuepusha matukio ya utekaji na mauaji ili kuepusha malalamiko ya wananchi.
Baadhi wametaka Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi isikwamishe uhuru wa wananchi kutoa maoni.
Maoni ya wadau
Waziri wa zamani na kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Anna Abdallah amesema hakukuwa na sababu ya Chadema kuvutana na polisi bali watafute amani kwa mazungumzo.
“Mimi ninachosisitiza ni amani. Huwezi ukafanya kitu chochote na mahali popote bila amani, lazima kuwe na amani na kama kuna tatizo watu wazungumze. Amani ndiyo msingi wa maendeleo. Kusipokuwa na amani watu wanajikuta mapangoni,” amesema.
Amesema hata kama Chadema wana madai ya msingi bado waangalie zaidi suluhisho.
“Hata kama watu wametekwa au wameuawa ndiyo unachukua bunduki unapiga? Ni lazima watu wazungumze, lazima kukaa pamoja. Amani, amani amani, lakini ukisema umeonewa ndiyo unakwenda kulipiza, unapokwenda ukikuta siyo kuzuri kwako, utafanyaje?” amehoji.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema alishafanya juhudi ya kushauriana na Chadema.
“Zipo taratibu nyingi za kufuata, hata mahakamani ni vivyo hivyo, mtu hakupigi na wewe ushike panga umpige. Ukishika panga umpige wote mnachukuliwa kuwa ni wahalifu tu wa jinai, lakini ukikimbilia mahakamani ukafungua kesi, anakamatwa anafunguliwa kesi,” amesema.
Amesema baada ya polisi kuzuia maandamano ya Chadema, walipaswa kufuata utaratibu wa kisheria.
“Tusipofuata utaratibu tutakuwa tunaingia kwenye vurugu na hilo sijasema kwamba Chadema wako sahihi au hawako sahihi au sijasema polisi wako sahihi au hawako sahihi.
“Lakini Polisi walipotoa taarifa yao kulikuwa na taratibu mbalimbali zingefuata hapo kabla tu ya kuingia barabarani,” amesema.
Sheria inasemaje?
Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi kifungu cha 43(1) inasema: “Mtu yeyote ambaye ana mpango wa kufanya, kukusanya, kuunda au kupanga mkusanyiko au maandamano ya hadhara, kwa muda usiopungua saa 48, kabla ya mkusanyiko au maandamano kwa muda uliopangwa kuanza, atawasilisha kwa maandishi notisi kuhusu kufanyika kwa mkusanyiko au maandamano hayo kwa ofisa polisi msimamizi wa eneo hilo.”
Kifungu hicho kinamtaka mwombaji kuainisha sehemu na muda ambao mkutano utafanyika, madhumuni kwa ujumla kuhusu mkutano huo na maelezo mengine kama Waziri atakavyotangaza kwa notisi.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu sheria hiyo, Mwanasheria Patience Mlowe amesema kuna changamoto ya maofisa wa polisi kuitafsiri sheria hiyo.
“Kinachotolewa si kibali, bali taarifa tu ya maandamano, sasa mara nyingi wakuu wa polisi wa wilaya wamekuwa wakiitafsiri vibaya notisi hiyo, wao wanaona wamepewa mamlaka ya kukubali au kukataa,” amesema.
Amesema sheria hiyo imekwenda mbali zaidi kwa kusema kama umenyimwa haki ya kufanya maandamano, inatakiwa ukate rufaa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani.
“Sasa polisi bosi wao ni waziri, kwa hiyo kuna mgongano wa masilahi hapo. Mara nyingi waziri anashauriwa na watendaji wanaohusika na hilo eneo na hapo ndipo waziri atarudi tena kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), ndiyo maana vyama vimekuwa havikati rufaa ya kufanya maandamano,” amesema.
“Kilichotakiwa jana (Septemba 23) ni Chadema kukata rufaa kwa waziri, akikataa ndio wafanye uamuzi mwingine, kwa hiyo wao waliamua kukatisha kwa kwenda moja kwa moja baada ya kukataliwa,” amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe, amesema yanayoendelea kwenye uwanja wa siasa yanadhoofisha waziwazi falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Falsafa ya 4R inahusisha Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahamiliivu), Reforms (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujanga Upya).
“Utakumbuka mara tu baada ya kuingia madarakani mwaka 2021, Rais alifungua ukurasa mpya wa kufanya siasa zenye msingi wa Maridhiano, Ustahamiliivu, Mabadiliko na Kujanga Upya.
“Ni dhahiri sasa kuwa kuna juhudi za baadhi ya makundi kufifisha kabisa siasa za kistaarabu ambazo kwa maoni yangu juhudi hizo zinajenga taswira mpya ya kutaka kuonyesha kuwa siasa ni chuki, uhasama na vurugu kitu ambacho siyo sahihi na wala si malengo ya Rais,” amesema.
“Kama jamii ya vyama vya siasa na wadau wanapaswa kukaa mezani kutatua changamoto hizi bila kutumia nguvu,” amesema.
Kwa upande wake, mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Luisuile amesema licha ya maandamano ya Chadema kuzuiwa na polisi ujumbe waliotaka kuufikisha umefanikiwa.
“Ujumbe wa Chadema umefika kwa sababu polisi wamejiandaa kikamilifu na kuzuia mitaa yote na maeneo yote ambayo yaliyokuwa yafanyike maandamano. Sasa uwepo wao pale na picha mbalimbali zilizopigwa hayo ni zaidi ya maandamano,” amesema.
Amesema picha za ulinzi wa polisi na kukamatwa kwa viongozi wa chama hicho zilisambaa mitandaoni duniani kote.
“Ni kweli kwamba wangepata nafasi wangezungumza na ingesikika zaidi, lakini hizo ndizo harakati zenyewe. Bado kwa vyovyote vile watu wamebaki na maswali, kwamba kuna nini? Kwa sababu kilichotokea ni doa kwa demokrasia,” amesema.
Dk Luisuile amesema Serikali ina wajibu wa kukomesha vitendo vya utekaji na mauaji.
Kuhusu maandamano
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Septemba 11, 2024 baada ya kufanya kikao na viongozi wenzake jijini Dar es Salaam walitaka Serikali itoe maelezo kuhusu matukio ya kutekwa na mauaji ya wananchi wakiwamo makada wa chama hicho, miongoni mwao akiwamo Ally Kibao aliyeuawa baada ya kutekwa ndani ya basi Dar es Salaam Septemba 6, 2024.
Maandamano hayo yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi Septemba 13, 2024 likieleza tayari Rais Samia ameshatoa maagizo ya kufanyika uchunguzi kuhusu matukio hayo.
Chadema iliweka msimamo wa kuandamana Septemba 23, na katika kudhibiti maandamano hayo, makada wa Chadema zaidi ya 50 walikamatwa, akiwemo Mbowe, Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema na makada wengine waliokamatwa maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam.
Hata hivyo, wengi waliachiwa kwa dhamana baada ya kukamatwa.
Hali mitaani
Jeshi la Polisi leo Septemba 24, 2024 limendelea na doria katika maeneo kadhaa ya Jiji la Dar es Salaam.
Mbali na hayo, askari wengine walizingira ofisi ya chama hicho iliyopi Mikocheni.
Mwandishi wa Mwananchi aliyefika katika ofisi hizo ameshuhudia hadi saa nane mchana askari baadhi wakiwa na silaha za moto wakirandaranda nje ya ofisi.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa askari hao, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema bado wanaendelea na kuimarisha ulinzi kama walivyofanya jana (Septemba 23).
“Tunaimarisha ulinzi tangu jana kwenye zile pointi muhimu hakuna tukio lolote la kijinai lililotokea wananchi wako salama. Polisi kuzingira ofisi za Chadema na wao tunawalinda kama wananchi wengine wakawaida maana hawakawii kusema wametekwa,” amesema Kamanda Muliro.
Ndani ya ofisi hiyo makada na maofisa, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika na Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Catherine Ruge walikuwepo wakiendelea na kazi zao.
Alipoulizwa kuhusu hatua ambazo Chadema wanachukua, Lissu amesema wanasubiri kufanya kikao kitakachotoka na tamko la pamoja.