Kauli ya RPC Geita itekelezwe pande zote

Kauli ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita (RPC), Saphia Jongo, inayowataka wananchi kutokubali kukamatwa na polisi wasiojitambulisha, imeleta mwangaza mpya kuhusu haki za raia na usalama, na inapaswa kutekelezwa katika mikoa yote ya Tanzania.

 Katika zama hizi za ongezeko la matukio ya utekaji yanayodaiwa kufanywa na watu wanaojifanya askari, kauli hii inakuja kama msaada mkubwa kwa wananchi wanaotafuta namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vya kihalifu vinavyovaa sura ya sheria.

Kamanda Jongo, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa mafunzo kwa viongozi wa mitaa na vijiji, alieleza wazi kuwa askari halali anapokwenda kumkamata mtu, ni lazima ajitambulishe kwa jina, awe na kitambulisho halali cha kazi na aeleze anatoka kituo gani cha polisi.

Ikiwa mtu anayedai ni askari hana sifa hizo, basi atakuwa si askari, bali anaweza kuwa mhalifu.

Kauli hiyo si tu inatilia mkazo uzingatiaji wa sheria, bali pia inalenga kuwapa wananchi uelewa wa haki zao, ili waweze kuchukua tahadhari na kuepuka kuwa waathirika wa matukio ya kihalifu yanayofanywa na watu wanaojifanya kuwa sehemu ya vyombo vya dola.

Uhalisia ni kwamba, hali ya wasiwasi imezidi miongoni mwa wananchi kutokana na baadhi ya watu kutumia sare za polisi na magari yanayodaiwa kuwa ya Serikali kufanikisha utekaji, bila kutoa uthibitisho wowote wa mamlaka yao.

Kama ambavyo kauli hiyo imeungwa mkono na wadau mbalimbali wa haki za binadamu na sheria, hata sisi tunaungana nayo tukisisitiza pia itumike kubadili mitazamo na hulka za askari polisi nchini.

Tunasema hayo kwa sababu sote ni mashuhuda wa jinsi hata askari wenyewe si wote wanaojitambulisha wanapokwenda kumkamata mtuhumiwa, na hata wanapotaakiwa kutoa utambulisho au kuonyesha hati ya upekuzi, hujibu kwa mabavu  na kejeli.

Yapo matukio mengi ambayo askari polisi wamewakamata watuhumiwa kwa kuwavamia majumbani au kwa njia nyingine bila kutaka hata ndugu zao wajue wapo kwenye vituo gani hadi wanapokuja kuibukia mahakamani.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiaji, kifungu cha 14(1), pamoja na Kanuni za Kudumu za Jeshi la Polisi (PGO), askari anayemkamata mtu anatakiwa kuwa na hati halali ya ukamataji, ajitambulishe, na amwambie mtuhumiwa tuhuma zinazomkabili.

Hivyo, askari polisi pia anapaswa kufuata sheria na utaratibu wa kushirikiana na viongozi wa eneo husika na kumruhusu mtuhumiwa kuwasiliana na ndugu zake.

Ni muhimu kwa viongozi wa polisi katika mikoa yote nchini kuiga mfano huu wa RPC Jongo kwa kusisitiza weledi na uwazi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuwafahamisha raia haki zao na wenyewe kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Hatua hii itarejesha imani ya wananchi kwa vyombo vya usalama na kusaidia kupambana na uhalifu kwa  njia ya haki, wazi na ya kisheria.

Ni wakati sasa kwa Jeshi la Polisi nchini kuimarisha elimu kwa umma kuhusu haki za raia wakati wa ukamataji na kuhakikisha kuwa kila askari anafuata misingi ya sheria.

Kwa kufanya hivyo, si tu kwamba tutaimarisha usalama, bali pia tutaijenga jamii inayotambua haki zake na kushirikiana kwa karibu na vyombo vya dola katika kulinda amani na usalama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *