Kauli ya Ramovic na kauli nyingine tata zilizozua mijadala

Kocha wa Yanga, Sead Ramovic, amezua mijadala kutokana na kauli aliyoitoa Jumamosi ya Januari 18, baada ya mchezo wa mwisho hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya MC Alger ya Algeria.

Kocha huyo ambaye aliingia kwenye mchezo hii akihitaji kushinda, alitoka patupu na kulalamikia udhaifu wa ligi ya Tanzania kama sababu ya timu yake kukosa ushindi.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, kocha huyo mwenye asili ya Serbia lakini raia wa Ujerumani,  alisema ligi ya Tanzania inakosa kitu kinachoitwa ‘intensity’ kulinganisha na ligi nyingine.

Intensity maana yake ni uharaka wa uchezaji na ufanyaji wa maamuzi kwa wachezaji uwanjani.

Ligi yenye intensity ndogo ni dhaifu, nyepesi na haina ubora, na hicho ndicho kilichowachefua watu wengi walioshiriki kwa namna moja au nyingine kutoa maoni yao.

Lakini kauli ya kocha hiyo siyo ya kwanza hapa nchini kuleta mijadala mikubwa kwenye michezo.

Zifuatazo ni kauli nyingine ambazo ziliwahi kutolewa na wadau wa michezo na kuleta mgawanyiko wa maoni miongoni mwa wanafamilia wa michezo hapa nchini.

Wachezaji wa Twiga stars wamefika kikomo – Mkwassa

Mwaka 2008 Charles Boniface Mkwassa aliteuliwa na TFF kuwa kocha wa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars.

Akaisaidia kufuzu kwa fainali za WAFCON 2010 zilizofanyika Afrika Kusini.

Baada ya mashindano hayo timu ikarudi kujiandaa na WAFCON ya 2012 iliyotakiwa kufanyika Guinea ya Ikweta.

Katika mchakato wa kufuzu, Twiga Stars ikakutana na Ethiopia kwenye hatua ya mwisho.

Mchezo wa kwanza ulifanyika ugenini na Twiga Stars kupoteza 2-1.

Matumaini yalikuwa makubwa nyumbani kwamba ushindi wa 1-0 ungetosha kwa Twiga Stars kufuzu fainali za pili mfululizo.

Lakini haikuwa bahati, Twiga Stars ikafungwa 1-0 na kupoteza matumaini ya Watanzania ya kufuzu.

Baada ya mechi, Mkwassa akaongea na vyombo vya habari na kusema wachezaji wa Twiga Stars wamefika kikomo. Kauli hii haikumuacha salama dhidi ya wadau wa soka la wanawake.

Mengi yakasemwa kumhusu Mkwassa kwamba yeye ndiyo amefika kikomo cha uwezo wake na wala siyo wachezaji. Kombora hili dhidi ya Mkwassa lilirushwa na Dkt. Maneno Tamba (sasa marehemu), mmoja wa wadau wakuu wa soka la wanawake wakati huo akiwa mmiliki wa timu ya Mburahati Queens na mwenyekiti wa chama cha soka la wanawake Dar es Salaam, alimshutumu Mkwassa kwamba yeye ndiye amefika kikomo.

Baada ya presha kubwa, Mkwassa akatangaza kujiuzulu.

Makocha wa kigeni tofauti yao na sisi ni rangi tu – Mecky

Kuelekea mchezo dhidi ya Simba SC, kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alihojiwa na vyombo vya habari kuhusu tofauti ya kiuwezo baina yake na mpinzani wake Abdellhak Benchikha.

Mecky akasema tofauti pekee kati ya makocha wa kigeni na wazawa ni rangi tu, lakini hakuna tofauti ya uwezo baina yao.

Kauli hii ilizua utata ikijadiliwa kimpira na kimaadili. Wengi walimuona Mecky kama ametoa kauli ya kibaguzi na kuanza kumkosoa, akiwemo mchambuzi wa Wasafi, Edo Kumwembe.

Mecky akasimamia kauli yake kwamba haikuwa ya kibaguzi bali uhalisia.

Mashabiki wa Yanga wala mihogo – Hersi

Hii ni kauli iliyotolewa na Rais wa Klabu ya Yanga,  Hersi Said, alipokuwa jijini Mwanza, Oktoba, 2022 katika ukumbi wa bwalo la jeshi alipokuwa akiongea na viongozi wa matawi ya wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kuelekea mchezo wao wa Ligi Kuu dhidi ya Geita Gold.

“Kuna mtu yeye kala zake mihogo huko, ‘sisi timu inatuuma zaidi”. Nyie viongozi nyie, sisi ndiyo tunaumia”.

Hersi aliwalenga mashabiki ambao kazi yao ni kulalamikia viongozi pale timu inapofanya vibaya, kana kwamba viongozi hawana uchungu na timu.

Kauli hii ilipokelewa vizuri sana tena kwa makofi bwaloni pale, lakini baada ya sare ya 0-0 nyumbani dhidi ya Club Africain, ndipo mapokeo yakabadilika.

Wale mashabiki wala mihogo ambao Hersi aliwalenga, wakageuza kibao na kurudisha mashambulizi kwa Rais wao.

Mapovu yakawatoka na ndipo wapinzani wao wakaidaka na kuteleza nayo kwa kuwaita Yanga wala mihogo.

Mashabiki wa Yanga wanalia kama nyani – Luc Aymel

Kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael, aligonga vichwa vya habari alipofananisha malalamiko ya mashabiki wa Yanga kuhusu timu yao na makelele ya nyani.

“Mashabiki wa Yanga hawana elimu, watu kwenye nchi hii ni(….), mashabiki hawajui mpira kazi yao ni kupiga kelele kama nyani na bata.

Viongozi wa klabu ni sifuri na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya Simba tu,”.

Kauli hii ikamponza na kufukuzwa kazi akiwa ameifundisha timu hiyo kwenye mechi saba tu.

Ratiba ya Ligi kama mafungu ya samaki – Aggrey Morris

Desemba 2019 Azam FC waliwakaribisha JKT Tanzania dimbani Zam Complex na kuambulia sare ya 2-2.

Mechi hii ilikuwa na mkanganyiko wa muda wa michezo, awali ilipangwa kufanyika saa moja usiku lakini baadaye ratiba ikabadilishwa na kuwa saa kumi jioni.

Nahodha wa Azam FC, Aggrey Morris, akiongea baada ya mchezo huo alilalamikia mabadilio hayo ya ghafla ya muda wa mchezo na kusema ligi haina utaratibu kama genge la samaki.

“Haiwezekani, siku sote unaambiwa mechi saa moja, na mnafanya mazoezi kujiandaa na mechi ya saa moja, na hadi mazoezi ya mwisho mmefanya saa moja.”

“Ghafla mnashitukizwa mnaambiwa mechi saa kumi, unapofanya mazoezi saa moja, hali ya hewa ya saa moja unakuwa umeizoea. Saa kumi jua kali tunashtukizwa. Tungeambiwa mapema kwamba mechi ni saa kumi tungefanya mazoezi saa kumi.

“Ratiba tunashitukizwa kama genge la samaki bwana.”

Kauli hii ilimtia matatani kwa mamlaka na kupewa onyo kali sana.

Morocco wanapendelewa na CAF – Adel Amrouche

Kocha wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Adel Amrouche aliingia kwenye mgogoro mkubwa na mamlaka ya soka Afrika (CAF) na baadaye waajiri wake (TFF) kwa kauli aliyoitoa kwenye AFCON 2023 iliyofanyika 2024 kule Ivory Coast.

Kuelekea mchezo wa kwanza wa Stars dhidi ya Morocco, Amrouche ambaye ni raia wa Algeria nchi yenye uhasama mkubwa kisiasa na Morocco, alisema wapinzani wake hao hufanya fitna za ndani kwa ndani ili kupata upendeleo kutoka CAF.

“Tunatambua nguvu za Morocco, ni wababe wa Afrika. Lakini tuliomba mechi yetu ianze saa nane mchana, tukalazimishwa kucheza usiku. Inaonekana katika mpira wa Afrika, ubade ndiyo huamua…na hatuna cha kufanya zaidi ya kupambana na wababe.”

Kauli hii ikamtia hatiani ambapo CAF walimfungia mechi nane, na baadaye kupoteza kazi kabisa.

Kushindana na makocha wanaume siyo haki – Edna Lema

Januari 2022, timu ya wanawake ya Yanga Princess ilifungwa 4-1 na wapinzani wa wa jadi, Simba Queens.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Yanga Princess, Edna Lema a.k.a Mourinho, alialamikia uwepo wa makocha wanaume kwenye benchi la wapinzani wao.

“Haiwezekani huku anafundisha mwanamke, huku mwanaume halafu utegemee usawa”

Lema aliyasema haya akilalamikia uwepo wa Mussa Hassan ‘Mgosi’ kama kocha mkuu wa Simba Queens.

Kauli hii haikupokelewa vizuri na mashabiki wa soka huku wengine wakihoji zile harakati za wanawake za haki sawa.

Wengine wakaenda mbali zaidi na kusema kama hoja ni kocha mwanaume, kwenye benchi lake naye pia alikuwa na kocha mwanaume kama msaidizi wake, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’.

Kauli zenye utata ni nyingi na hazijaanza na wala hazitoisha kesho. Lakini kikubwa kwa kauli ya Sead Ramovic ni kwamba siku chache baada ya kuitoa, ligi ya Tanzania ikapanda viwango kutoka ya sita hadi ya nne barani Afrika na ya 57 duniani, kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Soka (IFFHS).