
Kauli ya rais wa Kenya William Ruto kuhusu kurejea kwa wanaharakati waliotekwa nyara imezua ghadhabu miongoni mwa raia. Siku ya Jumatatu, Mei 12, wakati wa mkutano na wanahabari, rais wa Kenya alibainisha kwamba watu wote waliotoweka katika miezi ya hivi majuzi chini ya hali isiyoeleweka wameunganishwa tena na familia zao.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Nairobi, Gaëlle Laleix
William Ruto aliendelea kuhakikishia kuwa hakutakuwa na utekaji nyara au visa vya watu kutoweka wakati wa utawala wake. Mwaka mmoja baada ya maandamano dhidi ya sheria ya fedha, ambayo yalisababisha karibu vifo 60 na watu 80 kutoweka kutokana na ukandamizaji wa polisi, kauli hizi zinapokelewa shingo upande.
“Tunaona kauli hii si sahihi na ni ya dharau kwa familia za Wakenya zinazoendelea kuwatafuta wapendwa wao,” Vocal Africa imeandika katika taarifa. Shirika hili la kutetea haki za binadamu limechapisha orodha ya majina ya watu ambao hawajapatikana, wengi wao walitoweka wakati wa maandamano ya mwezi Mei na mwezi Juni 2024. “Majina haya yanawakilisha sehemu ndogo tu ya mfumo mkubwa wa ukandamizaji na kutokujali,” Vocal Africa inaongeza.
Kauli ya rais Ruto “haikubaliki”
David Maraga, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya anasema matamshi ya William Ruto “hayakubaliki, wakati bado kuna miito mingi kwa mahakama.” Siku ya Jumapili, Siku ya Akina Mama, wazazi wa waathiriwa wa ukandamizaji wa maandamano dhidi ya sheria ya fedha walichapisha ombi la kutaka mwanga utolewe kuhusu hatima ya watoto wao.
Uhuru hatarini
“Sasa kwa vile William Ruto anakubali utekaji nyara,” ameandika kiongozi wa upinzani Martha Karua kwenye ukurasa wake wa mtanado wa kijamii wa X, “lazima pia atambue hukumu ya kifo na jukumu la vikosi vya usalama katika haya yote.” Mnamo Mei 1, wakati wa ukaguzi wake wa mara kwa mara, Kenya ilinyooshewa kidole cha lawama na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Kibinadamu, ambayo ilishutumu hasa ghasia za polisi na kukandamizwa kwa uhuru wa raia.