
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile, ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Novemba 27, 2024, nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu, aliwaacha Watanzania na ujumbe mzito wa maono na matumaini alipohitimisha hotuba yake ya mwisho bungeni.
“Nimepewa miezi sita kujipanga na kuandaa maono yangu nitakapoanza kazi Machi mwakani. Nia ya kufanya hivyo ninayo, sababu za kufanya hivyo ninazo na uwezo wa kufanya hivyo ninao,” alisema Dk Ndugulile kwa imani na msisitizo bungeni jijini Dodoma Septemba 3, 2024.
Hotuba hiyo ilikuwa ni kutokana na kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi kikanda wa Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO), katika kikao cha 74 cha Kamati ya Kanda ya Afrika ya shirika hilo kilichofanyika nchini Congo Brazzaville Agosti 26 hadi Agosti 30, 2024 na alitarajiwa kumrithi Dk Matshidiso Moeti wa Botswana aliyemaliza muda wake.
Aliwahimiza wabunge na Watanzania wote kuendelea kumwombea na kumsapoti katika kipindi cha mpito, akisema nafasi aliyokuwa nayo ilibeba matarajio makubwa kutoka kwa Watanzania na Waafrika kwa ujumla.
Kauli hiyo sasa inabaki kuwa kumbukumbu ya maono yake makubwa na dhamira ya dhati ya kulitumikia Taifa kwa bidii na maarifa.
Endelea kufuatilia Mwananchi.