Dar es Salaam. Kocha wa Simba, Fadlu Davids ametoa maoni yake muda mfupi baada ya timu yake kupangwa kukutana na Al Masry katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.
Katika hatua hiyo, Simba itaanzia kwa kucheza ugenini kati ya Aprili Mosi hadi 2 mwaka huu na mechi ya marudiano itachezwa hapa Dar es Salaam kati ya Aprili 8 hadi 9, 2025.

Timu itakayopata matokeo mazuri baina ya Simba na Al Masry, itakutana na mshindi wa mechi baina ya Stellenbosch ya Afrika Kusini na Zamalek ya Misri.
Fadlu amezungumzia mambo matatu kuhusu mechi yao dhidi ya Al Masry.

Wapinzani wagumu
Davids amesema timu yake inafahamu kwamba Al Masry ni timu ngumu kama ambavyo ingekuwa dhidi ya timu nyingine yoyote ambayo wangekutana nayo hivyo watahakikisha wanajiandaa vizuri.
“Tulitegemea droo na timu yoyote ambayo tungecheza nayo ingekuwa ni ngumu. (Al Masry) wanafanya vizuri katika Ligi Kuu ya Misri na itakuwa mechi ngumu hasa tutakapokuwa kwao Misri,” amesema Fadlu.
Katika Ligi ya Misri, hadi sasa Al Masry inashika nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 23 huku Pyramids ikiongoza ikiwa imekusanya pointi 33.

Hesabu ugenini
Fadlu anafahamu kuwa Al Masry ni timu sumbufu inapokuwa katika Uwanja wa nyumbani lakini anaamini uzoefu ambao Simba inao kwa mazingira na soka la Misri utawapa faida.
“Tumekaa kambi ya maandalizi ya msimu kule Misri hivyo tumejiandaa vizuri na hali ya hewa ya kule na tumecheza dhidi ya timu za kule. Haitakuwa mechi rahisi kama ilivyo kwa nyingine lakini tuko tayari kwa mchezo,” amesema Fadlu.
Katika mechi nne za kimataifa ambazo Simba imecheza ugenini msimu huu, imepata ushindi mara moja, kutoka sare mbili na kupoteza moja.Imefunga mabao matatu na imeruhusu mabao matatu.

Kazi maalum kwa mashabiki
Kocha Fadlu Davids amesema kuwa ushindi na matokeo mazuri katika mechi ya nyumbani yatachangiwa kwa kiasi kikubwa na mashabiki hivyo wanapaswa kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono timu katika mchezo ambao Simba itakuwa nyumbani.
“Kuongoza kundi ni jambo zuri hivyo unacheza ugenini kwanza na kwa matokeo unajua nini cha kufanya, nini cha kutegemea na matokeo gani unahitaji na kwa mashabiki ambao watakuwa nyuma yetu katika mechi ya Dar es Salaam wanatupa faida katika mechi ya pili,” alisema Fadlu.
Historia inaonyesha kuwa hii itakuwa ni mara ya pili kwa Simba na Al Masry kukutana katika Kombe la Shirikisho Afrika ambapo mara ya kwanza ilikuwa ni 2018 katika raundi ya kwanza ya mashindano hayo.
Mwaka huo 2018, Simba ilitolewa kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya mechi mbili baina yake na Al Masry kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2 na mechi ya marudiano huko Cairo Misri ilimalizika kwa sare tasa.