Katika muda wa siku moja, jeshi la Kizayuni lafanya mashambulio 145 nchini Lebanon

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limefanya mashambulizi 145 nchini Lebanon katika muda wa saa 24 zilizopita huku likishaidisha hujuma zake za kinyama dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu kinyume na wito wa kimataifa wa kuutaka utawala huo haramu usimamishe mashine yake ya mauaji katika eneo hili la Asia Magharibi.

Katika ripoti aliyotoa mapema leo, Waziri wa Mazingira wa Lebanon Nasser Yassin amesema mashambulio mengi ya utawala ghasibu wa Israel yamelenga maeneo ya Kusini mwa Lebanon, yanayojumuisha majimbo ya Kusini na Nabatiyeh.

Ripoti hiyo imebainisha utawala wa Kizayuni umefanya jumla ya mashambulizi 13,222 tangu ulipoanzisha hujuma zake dhidi ya Lebanon katika kipindi cha miezi 13 iliyopita.

Mashambulio ya makombora ya Hizbullah dhidi ya ngome za Israel

Wakati huo huo, Shirika la Taifa la Habari la Lebanon (NNA) limeripoti kuwa ndege za kivita za Israel zimeharibu jengo la makazi la ghorofa 12 katika kitongoji cha Chiyah, kusini mwa mji mkuu Beirut.

Aidha, limeripoti mashambulizi makali ya anga yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni kwenye vitongoji vya Burj al-Barajneh na Hadath mjini Beirut.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, shambulio la anga dhidi ya Hadath lilipiga karibu na Hospitali ya Saint George.

Mashambulizi hayo ya kinyama ya jeshi la utawala haramu wa Israel yamefanywa baada ya harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon kutekeleza kwa mafanikio operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya kambi tano kuu za kijeshi za Israel katika mji wa Haifa na viunga vyake katika sehemu ya kaskazini ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel…/