Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limethibitisha kuangamizwa wanajeshi wake 10 kusini mwa Lebanon huku idadi ya vifo vya askari hao ikiongezeka kutokana na operesheni za kulipiza kisasi zinazotekelezwa na wanamuqawama wa Hizbullah dhidi ya wavamizi hao.
Shambulio la hivi punde la Hizbullah lilikuwa la kuvizia lililowalenga wanajeshi wa vita wa Kizayuni kusini mwa Lebanon na wengine waliokuwa wakifanya kazi za kilojistiki za kusambaza vifaa kwa askari wenzao.
Katika shambulizi hilo, wanajeshi watano wa Kizayuni waliangamizwa na wengine 24 walijeruhiwa, wakiwemo wanne ambao hali zao ni mahatuti.
Wanajeshi wote waliouawa walihudumu katika Kikosi cha 89 cha Brigedi ya 8, na imeelezwa kuwa waliangamizwa na kombora la Hizbullah katika kijiji kimoja cha kusini mwa Lebanon.

Taarifa za kuangamizwa wanajeshi watano wa Israel zimetolewa chini ya saa 24 baada ya jeshi la utawala huo wa Kizayuni kuthibitisha kuuawa wanajeshi wake wengine watano katika shambulio lililofanywa na Hizbullah.
Kutokana na uchujaji na udhibiti mkali wa habari za kijeshi unaofanywa na Israel, taarifa za kuangamizwa askari hao zimethibitishwa na jeshi la utawala huo mapema leo.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, zaidi ya wanajeshi 70 wa Israel wameshaangamizwa hadi sasa na wengine zaidi ya 600 wamejeruhiwa tangu jeshi hilo lilipoanzisha uvamizi dhidi ya ardhi ya Lebanon mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba.
Huku kukiwapo na ongezeko la idadi ya wanajeshi wanaouawa, mkuu wa majeshi ya Israel Herzi Halevi amedokeza kuhusu uwezekano wa “kuhitimisha” vita na Hizbullah…/