Septemba 2020 Harmonize alivunja kibubu chake na kufanya usajli wa kutisha kwa ajili ya kumarisha kikosi kazi chake cha Konde Music Worldwide. Lebo hiyo ilifanikiwa kunasa saini za Country Boy, Cheed na Killy ambao walijumuika kikosini na Ibraah na Skales kutokea Nigeria.
Baada ya Harmonize kufungua Konde Music, lebo hiyo ilianza kupambanishwa sana na WCB Wasafi yake Diamond Platnumz ambayo ndio ilimleta Harmonize katika ulimwengu wa muziki na watu kumfahamu.
Kitendo cha Harmonize kusaini wasanii watatu (Country Boy, Cheed na Killy) kwa wakati mmoja, ulikuwa ni mfano wa mjumbe aliyetumwa kupeleka salamu kwa mabosi wake hao wa zamani, WCB Wasafi, kwamba wapo tayari kwa mapambano.
Konde Music ikiwa inaelekea kutimiza mmoja na nusu kwa wakati huo, tayari ilikuwa na idadi sawa ya wasanii na WCB Wasafi ambayo ilianza kusaini wasanii tangu 2015 Harmonize akiwa wa kwanza kumwaga wino.

Ukimtoa Diamond kama kiongozi, WCB ilikuwa na Rayvanny, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso na Zuchu. Hao jumla yao ni watano. Kwa upande wa Konde Music ukimtoa Harmonize kama kiongozi kulikuwa na Ibraah, Skales, Country Boy, Cheed na Killy. Pia hao jumla yao ni watano.
Ili salamu hizo ziwe zenye heri zaidi, Harmonize aliwapatia magari Country Boy na Ibraah ambao aliwasaini kwa mwaka huo. Hapo tayari Diamond naye alikuwa amempatia Zuchu gari ikiwa ni takribani miezi sita tangu atangazwe kuwa chini ya WCB Wasafi.
Kitendo cha Harmonize kusaini wasanii wengi kwa wakati mfupi kilikosolewa vikali na baadhi ya watu akiwemo meneja wa Diamond na WCB Wasafi, Sallam SK. Hoja ilikuwa ni kwamba ni vigumu kuwasimamia wote kwa wakati mmoja na kufanya vizuri katika soko la ushindani.
Ndicho kilichokuja kutokea. Januari 2022 Konde Music walitangaza kuachana na Country Boy kwa kile walichoeleza ni kumalizika kwa mkataba wake na kumtakia kila la heri, miezi tisa mbeleni, Konde Music ikatangaza tena kuachana na wasanii wake watatu Cheed, Killy na Anjella, huku Skales akiwa haonekani tena kwenye lebo hiyo.
Kwa sasa Konde Music ukimtoa Harmonize imesaliwa na msanii mmoja ambaye ni Ibraah. Kwa muktadha huo, kama Konde Music walipanga kushindana na WCB Wasafi kwa idadi ya wasanii tayari wameshindwa pambano hilo.
Ndani ya WCB Wasafi ukimtoa Diamond kama mmiliki wa lebo bado kuna wasanii watano ambao ni Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice.

Ni wazi Konde Music imepotea katika ushindani na WCB Wasafi baada ya kujikuta imesalia na msanii mmoja tu ambaye ni Ibraah ambaye naye ukuaji wake haujawa wa kasi kama ambavyo ilitarajiwa na wengi hapo mwanzo.
Kitendo cha Konde Music kuachana na wasanii wake watano ndani ya muda mfupi, ilitarajiwa itakuwa ndio mwisho kwa Harmonize kushindana na Diamond au kumpunzisha katika mambo yake na ndivyo imekuwa hivyo.

Kwa sasa humsikii akimpiga tena vijembe katika nyimbo zake kama alivyofanya hapo awali katika nyimbo zaidi ya tano. Hana nguvu tena ya kumkosoa katika jambo lolote kuhusu uendeshaji wa lebo, ametulia maana kitu amejifunza.