Katika hatua ya kushangaza, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nchini Tanzania Freeman Mbowe ametangaza rasmi kuwa chama hicho hakitashiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mbowe amewataka viongozi wote wa Chadema na wanachama wao kutoshiriki uchaguzi huo akisisitiza kwa kusema “viongozi wote wa chama wasishiriki kwa njia yoyote katika uchaguzi huu”.
Tamko hilo la Mbowe linaashiria mkakati wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania wa kuondoa ushiriki wake katika uchaguzi huo, huku wakijaribu kueleza msimamo wao wa kisiasa katika mazingira ya sasa.
Mwenyekiti wa Chadema amefafanua kwa kusema: “katika hatua hii, tunajitoa katika uchaguzi, na tumechelea sana kuwaruhusu vijana wetu wapige kura”.

Uamuzi huo wa Chadema umetangazwa huku chama hicho kikikumbwa na changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na kushindwa kukusanya nguvu za vijana katika uchaguzi.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa nchini Tanzania unatazamiwa kufanyika tarehe 27 ya mwezi ujao wa Novemba, ambapo kampeni za uchaguzi huo zitaanza tarehe 20 na kuendelea hadi tarehe 26 Novemba.
Nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo ni za Wenyeviti wa Mitaa na wajumbe watano, ambao wawili kati yao watakuwa ni wanawake.
Uchaguzi huo unatafsiriwa kama kioo cha kuakisi muelekeo wa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2025 na kufanyika uchaguzi huo katika mazingira huru na ya haki…/