
Simiyu. Mahakama ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imemuhukumu kwenda jela miaka 20 Katibu wa Chama Cha Ushirika cha Msingi (Amcos) Kijiji cha Gula, wilayani humo, Masanja Mboje (36) baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya rushwa na uhujumu uchumi.
Mboje pia ameamriwa kurejesha Sh3.3 milioni ambazo alizifanyia ubadhirifu ikizingatiwa kuwa kati ya Sh3.5 milioni alikuwa tayari amerejesha Sh200,000.
Hukumu hiyo imetolewa leo Jumanne Mei 20, 2025 na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Aziz Hamis baada ya mshtakiwa kukiri makosa yake kulingana na hati ya mashitaka katika kesi ya uhujumu uchumi.
Katibu huyo kwa mujibu wa hati ya mashitaka alifikishwa mahakamani hapo Januari 3,2025 akishtakiwa kwa makosa wawili ufujaji na ubadhilifu wa fedha kinyume na Kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura 329 Marejeo ya Mwaka 2019, kikisomwa pamoja na aya ya 21 jedwali la kwanza pamoja na vifungu vya 57(1)na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa sura 200 Marejeo ya mwaka 2022.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Wilaya ya Maswa, Bahati Madoshi ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa akiwa Katibu wa Amcos ya Gula na mtu pekee aliyekasimiwa mamlaka ya kununua pamba kutoka kwa wakulima alitumia kwa matumizi yake binafsi Sh3.5 milioni ambazo alipaswa kumlipa Edward Mathias baada ya kupeleka pamba yake yenye uzito wa kilo 2,268.
Ameendelea kuieleza Mahakama kuwa kwa kufanya hivyo alikiuka mwongozo namba 1 wa msimu wa mwaka 2024/2025 kuhusu mfumo wa usimamizi na uuzaji wa pamba uliotolewa kwa Sheria ya tasnia ya pamba namba 2 ya mwaka 2011 unaotolewa na Bodi ya Pamba Tanzania.
Baada ya Mahakama kumtia hatia mshtakiwa, kabla ya hakimu kumsomea hukumu, alitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea ambapo aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu kwa kuwa ni mgonjwa na ana mke na watoto wanaomtegemea.
“Kwa hiyo Mahakama inakutia hatia mshtakiwa Masanja Mboje kwa makosa uliyoshtakiwa nayo, Mahakama hii inakuhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela, pia kulipa Sh3,318,000 milioni ambazo ulizifanyia ubadhilifu.”