
Mbeya. Simanzi imeibuka tena jijini Mbeya baada ya kifo cha aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), Mkoa wa Mbeya, Lucia Sule kufariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya.
Kifo hicho kinafanya kufikia jumla ya vifo sita katika ajali iliyotokea Februari 25, 2025 katika eneo la Shamwengo wilayani Mbeya wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Rajabu.
Ajali hiyo ilihusisha gari la Serikali STM na basi kampuni ya CRN ambapo mbali na vifo hivyo, watu saba walijeruhiwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu.
Katika ajali hiyo, watu watatu walifariki dunia papo hapo wakiwa ni mwandishi wa kujitegemea Furaha Simchimba, mjumbe wa kamati ya utekelezaji CCM Wilaya ya Mbeya, Daniel Mselewa na Utingo wa basi, Isaya Geazi ambao waliagwa Februali 27, 2025 jijini Mbeya.
Hata hivyo, vifo viliongezeka baada ya dereva wa gari la Serikali mkoani Mbeya, Thadei Focus kufariki dunia akipatiwa matibabu sawa na mwandishi wa Dream Media, Seleman Ndelage na kufikia watano waliofariki dunia.
Idadi imeongezeka tena na kufikia sita baada ya Lucia naye kufariki dunia akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya huku majeruhi wawili, mwandishi Epimarcus Apolnali wa Chanel Ten na Denis George wakiendelea na matibabu nyumbani baada ya kuruhusiwa kutokana na afya zao kuimarika.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Mbeya, Christopher Uhagile amethibitisha kifo hicho akieleza ni masikitiko makubwa kumpoteza kiongozi huyo aliyekuwa mchapakazi.
“Leo tutaendelea na maombolezo ambapo kesho Jumatano tutamuaga rasmi kisha kusafirishwa kwenda nyumbani kwao Babati mkoani Manyara, hili ni pigo kubwa kwa chama na Taifa kwa ujumla,” amesema na kuongeza:
“Tutamkumbuka kwa mengi, uchapakazi wake, misimamo na mpenda haki, CCM itashiriki vyema katika taratibu zote na tutausindikiza mwili hadi nyumbani kwao,” amesema Uhagile.