Katibu Mkuu wa UN: Dunia ichukue msimamo madhubuti dhidi ya mauaji ya kimbari huko Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuwepo msimamo mkali wa kimataifa dhidi ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameyasema hayo kando ya mkutano wa bioanuwai wa COP16 nchini Colombia na kuonya kwamba, iwapo jamii ya kimataifa haitachukua msimamo madhubuti wa kukomesha mgogoro wa Gaza, Tel Aviv itaendeleza mauaji ya kimbari huko Gaza.

Kauli ya Guterres imekuja baada ya mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika mji wa Beit Lahia, kaskazini mwa Gaza, siku ya Jumanne ambayo yameua shahidi raia wasiopungua 93 wa Palestina.

Wakati huo huo, ripoti zinaonyesha kupungua sana upelekaji wa misaada ya kibinadamu huko Gaza, suala ambalo limechochea uvumi kuwa Israel ina nia ya kuwafukuza Wapalestina waliosalia kutoka Ukanda wa Gaza.

Kuhusu suala hili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, yumkini lengo ni kuwalazimisha Wapalestina kuondoka Gaza ili wengine walikalie kwa mabavu eneo hilo.

Karibu Wapalestina elfu hamsini wameuawa katika kampeni ya mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na Isarel eneo la Ukanda wa Gaza tangu zaidi ya mwaka mmoja uliopita.