Katibu Mkuu wa UN aionya Israel: Kushambulia askari wa UNIFIL inaweza ikawa jinai ya kivita

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameutahadharisha utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, kuwashambulia walinda amani wa umoja huo kunakiuka sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za kimataifa za kibinadamu na kwamba ukiukaji huo unaweza kuwa uhalifu wa kivita.

Guterres ametoa indhari hiyo kufuatia uvunjaji wa makusudi wa sheria katika kituo cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani uliofanywa na magari ya kivita ya jeshi la utawala haramu wa Israel IDF kusini mwa Lebanon.

Tukio hilo lilitokea jana asubuhi saa za Lebanon wakati vifaru viwili vya IDF Merkava vilipoharibu lango kuu na kuingia kwa nguvu katika kituo hicho cha Umoja wa Mataifa.

Askari wa UNIFIL

Takriban saa mbili baadaye, baada ya vifaru hiyvo kuondoka, makombora kadhaa yalirushwa karibu na hapo, yakitoa moshi uliowaathiri walinda amani waliokuwa ndani.

Matukio hayo yamefuatia matukio kadhaa ya ukiukaji usalama yaliyotokea hivi karibuni yakihusisha jeshi la Kizayuni yakiwalenga askari wa vikosi vya amani vya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa mjini New York Katibu Mkuu Guterres amesisitiza kwamba ulinzi na usalama wa wafanyakazi na mali za Umoja wa Mataifa lazima uhakikishwe na kwamba kutofanywa ukiukwaji wowote dhidi ya majengo ya Umoja wa Mataifa…/